WATANZANIA kwa sasa wanaendelea kutazama uhondo wa michuano ya kimataifa ile ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na kuwa na timu mbili katika michuano hiyo ambayo inasimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Tanzania inawakilishwa na Simba ambao wapo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na jana Jumanne walikuwa na mechi ya hatua ya makundi walipokuwa wanacheza na Wasudan Al Merrikh ukiwa mchezo wa marudiano baina ya timu hizo baada ya ule wa kwanza kule Sudan.
Dakika 90 zilikamilika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 na kuwafanya wabaki na pointi tatu kisha wamefikisha jumla ya pointi 10 wakiwa ni namba moja kwenye kundi A.
Lakini kwenye Kombe la Shirikisho,
Tanzania wana wawakilishi ambao ni Namungo. Klabu hiyo nayo ipo hatua ya
makundi ya kombe hilo ambapo wao wana kibarua leo Jumatano dhidi ya Pyramids ya
Misri.
Huu ni mchezo wa pili kwa Namungo
wanaotokea Lindi baada ya kupoteza mbele ya Raja Casablanca mapema wiki
iliyopita kwa bao 1-0. Japo walifungwa lakini Namungo wana nafasi ya
kurekebisha makosa na kupita kwenye hatua hii ya makundi ambayo wapo kwa sasa.
Wakati leo Jumatano wanapambana na
Pyramids kuna kitu nataka kuwakumbusha Namungo ambacho kinaweza kuwa faida kwao
hasa katika nafasi ya kusonga mbele katika hatua hiyo ya makundi.
Kitu ambacho wanatakiwa kukichukua
na kukifanyia kazi wauaji hawa wa Kusini ni kupita kwenye njia ambayo iliwapa
mafanikio Simba kwa msimu wa 2018/19 ya kufanya vizuri wakiwa nyumbani.
Tayari wameshapoteza pointi tatu
katika mechi yao ugenini kule Morocco lakini wanachotakiwa kukifanya Namungo
leo ni kutokukubali kupoteza pointi lakini hata kwenye mechi zao mbili zaidi
ambazo watacheza nyumbani.
Hali hiyo itawasaidia kwa sababu
watakuwa na uhakika wa kukusanya pointi tisa wakiwa nyumbani ambazo kwa msimu
wa 2018/19 ndizo ziliwabeba Simba na kutinga hatua ya robo fainali ambapo
walikutana na TP Mazembe.
Kwenye michuano hii ni ngumu sana
kupata pointi unapokuwa ugenini kutokana na mazingira ya soka lenyewe la
Kiafrika lakini Namungo wanatakiwa kutumia ile faida ya kucheza wakiwa nyumbani
na kubeba pointi zote katika michuano hii.
Kwa sasa hesabu za Namungo
zinatakiwa kuanza kuchukua pointi kwa Pyramids leo Jumatano kwa ajili ya kuanza
kusafisha njia ya kufika robo fainali lakini baada ya hapo ni kwenye mechi
mbili zijazo dhidi ya Raja na Nkana FC.
Hesabu za kuweka akilini kwamba
Namungo wanaweza kuchukua pointi wakiwa ugenini hasa katika hatua hii nafikiri
kwanza ziwekwe kando licha ya kwamba timu yoyote inaweza kupata matokeo katika
mazingira yoyote ile. Nasema kuchukua pointi ugenini kutawapoteza Namungo kwa
sababu ya wapinzani ambao wamepangwa nao kuwa wataalamu wa kumaliza shughuli kila
wanapocheza nyumbani kwao.
Kwa wakati huu nawasihi sana
Namungo kufikiria sana namna ya kusaka pointi nyumbani ambazo zitawapa uhakika
wa kufika mbali wanapopataka kuliko kufikiri wanaweza kushinda na ugenini.
Lengo la kwanza liwe kushinda nyumbani kisha ikitokea ugenini basi iwe ziada.








Kwa maana hiyo simba ni kioo cha jamii
ReplyDelete