TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo Machi 28 imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Libya kwenye mchezo wa kuwania kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, (Afcon) uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
Bao pekee la ushindi kwa Stars lilipachikwa kimiani na Simon Msuva dakika ya 45+1 kwa kichwa akiwa ndani ya 18 na kuwafanya wachezaji na benchi la ufundi kunyanyuka kwa furaha.
Bao hilo lilidumu mpaka dakika 90 licha ya kipindi cha pili Libya kufanya mashambulizi makali matatu yaliokolewa na kipa Aishi Manula huku Stars wakiwa na kazi ya kulinda lango katika dakika za lala salama kwa kuwa wapinzani wao waliwaandama mwanzo mwisho.
Licha ya Stars kushinda imeongeza pointi zake tatu na kufikisha jumla ya pointi 7 ndani ya kundi J ila haina nafasi ya kufuzu Afcon kwa kuwa tayari Tunisia inayoongoza kundi ikiwa na pointi 13 na Equatorial Guinea yenye pointi 9 zimeshakata tiketi ya kwenda Cameroon.
Libya wao wamebaki na pointi tatu kwenye msimamo na pointi zao ni tatu baada ya kucheza jumla ya mechi sita.
Jitihada za nahodha wa Stars, Mbwana Samatta na Ayoub Lyanga kupata bao la pili ziligonga mwamba kipindi cha pili kwa kuwa Libya waliweka ukuta chuma ambao uliwapa shida Tanzania kupenya.
0 COMMENTS:
Post a Comment