ZAWADI kubwa ambayo kwa sasa mashabiki wanahitaji kutoka kwa wachezaji wao ni matokeo mazuri kila wakati. Hakuna kingine ambacho mashabiki wanahitaji.
Mwenye kazi ya kuwapa matokeo mazuri ni
mchezaji hivyo kazi yake ni lazima iwe kusaka ushindi. Dakika 90 zina maamuzi
hayo na ili ifanikiwe ni lazima kuwe na juhudi bila kukata tamaa.
Haijalishi ni mechi ya kirafiki ama
ushindani ni jambo moja linatafutwa ushindi baada ya mpira kukamilika masuala
ya kusema kwamba bahati mbaya huwa inawaumiza mashabiki.
Kushindwa kupatikana kwa matokeo kwenye
mchezo wa kwanza inapaswa iwe somo kwa ajili ya mechi inayofuata. Lakini jambo
la msingi kwa wachezaji ni kutambua kwamba zawadi inayohitajika ni ushindi.
Ipo wazi kwamba kwa msimu wa 2020/21
ushindani ni mkubwa na kila timu inajua kwamba inajukumu la kutimiza katika
kuyafikia malengo.
Kwa timu ambazo bado hazijawa na mwendo
mzuri ni muhimu kwa sasa kufanya kazi ya kurekebisha makosa ambayo wameyafanya.
Kwa timu ambazo matokeo yamekuwa ni ya
kusuasua ni muhimu kuongeza nguvu. Ikiwa zitakwama kubadili mwendo matokeo
yatakuwa tofauti mwisho wa mzunguko wa pili.
Inawezekana kwa kila timu kuweza kuwa
kwenye mabadiliko na kupata matokeo ambayo ni mazuri. Njia pekee ya kufanya
hivyo ni kufanya maandalizi mazuri.
Maandalizi yakiwa bora inakuwa rahisi
kupata matokeo chanya. Kila mchezaji anapoingia uwanjani huwa anafikiria
ushindi ikiwa hajapitia maandalizi mazuri itakuwa ngumu kufikia azma hiyo.
Jambo la msingi ambalo kwa sasa wachezaji
wanatakiwa kufanya ni kuongeza akili zaidi kupambania timu zao.
Kwa msimu huu ni timu nne ambazo zitakuwa
kwenye nafasi nne za mwisho zitashuka daraja. Pia mbili ambazo zitakuwa kwenye
nafasi ya 13 na 14 zitacheza playoff.
Hakuna ujanja wa kukwepa hatua hizi kwa
kuwa ligi inaendelea na matokeo lazima yaonekane. Ili kukwepa haya kwa timu
ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja kazi ni moja kupambana muda wote.
Matokeo mazuri yanahitajika kwa timu ambayo
inahitaji kubaki kwenye ligi. Pia kuna vita ya kusaka ubingwa wa ligi pamoja na
ile 10 bora.
Hali hii ni nzuri kwa sababu inafanya
ushindani unazidi kuongezeka kila wakati uwanjani. Ikiwa kutakuwa na kasi
kwenye ligi tutapata wachezaji wengi wazuri ambao watapata nafasi ya kuwa
kwenye timu ya taifa.
Habari kubwa kwa timu za Ligi Daraja la
Kwanza nao pia ni vita yao ya kuhitaji kushiriki Ligi Kuu Bara. Hapa nao vijana
wanapambana kutimiza malengo ambayo wanayo katika timu.
Inawezekana na muda ni sasa wa kuweka
mipango kwa umakini. Wakati wa kupanga kwamba kuna kupanda basi ikumbukwe
kwamba kuna kushuka pia ikiwa itaboronga.
Kwa kufanya hivyo itakuwa ni rahisi
viongozi kuweza kujipanga kwa ajili ya wakati ujao pale ambapo zitashuka
daraja. Kikubwa ni kwamba ukipanda unapaswa ujiandae pia kushuka.
Shukrani pia kwa mashabiki ambao wamekuwa
wakijitokeza uwanjani kuzipa sapoti timu zao zikiwa kazini. Katika hili pongezi
wanastahili.
Kwa sasa ambacho kinatakiwa ni kila shabiki
kuwa mstahimilivu pale matokeo yanapokuwa sio zawadi kwa upande wao. Maana yake
ni kwamba ikiwa hiyo zawadi haiwahusu basi wapo ambao wanahusika kuichukua.
Utulivu wao utawafanya waiepushie timu yao
na adhabu ambazo zimekuwa zikitolewa kutoka Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF).
Pia itawafanya wachezaji kujua kwamba
wamekosea kutoa zawadi ya maumivu wanapaswa kutoa zawadi ya furaha kwa
mashabiki wakati ujao.
Kushindwa kupata matokeo mechi moja haina
maana kwamba hakutakuwa na mechi nyingine hapana. Ni muhimu kujipanga kila
wakati kufanya vizuri.
Imani yangu ni kwamba wachezaji wanatambua
majukumu yao na mashabiki pia wanajua wanachotakiwa kukifanya wawapo uwanjani.
Kama kila mmoja anajua jukumu lake basi rai
yangu kusiwe na ugomvi katika kusaka ushindi hata pale ushindi utakapokosekana
baada ya dakika 90.
Maana kwa mechi za hivi karibuni nimekuwa
nikishuhudia matukio ambayo si salama kwa afya za wachezaji kutokana na faulo
ambazo wanachezeana bila kujali.
Jambo la msingi ni kuona kwamba mzunguko
huu wa pili yale makosa ambayo yalikuwa yanafanyika yanapunguzwa ama kuachwa
kabisa.
Mzunguko wa pili ushindani wake ni mkubwa
kuliko ule wa kwanza. Sababu ni kwamba wakati huu ni muda wa kukamilisha hesabu
kwa timu zote.
Rai yangu kwa wachezaji kuwa walinzi wa
wengine ndani ya uwanja na kujali afya za wenzao ili wawe salama mpaka pale
mpira utakapokamilika.
0 COMMENTS:
Post a Comment