April 15, 2021


UKIZITAZAMA mechi saba zilizochezwa na vinara wa ligi hivi karibuni Yanga siyo siri kwamba ina mwendo usioridhisha kwa sasa kwenye Ligi Kuu Bara. Hilo liko wazi na linaonekana dhahiri kwa mechi zake zilizopita.

Katika mechi hizo chini ya makocha watatu kwa maana ya Cedric Kaze na msaidizi wake Nizar Khalfan na sasa Juma Mwambusi, Yanga wameshinda moja, wamefungwa moja na sare tano

Kwa maana hiyo wameokota pointi nane kwenye 21 ambazo wamezigombea kwenye mechi hizo saba.

Huu siyo mwendo mzuri kwao kwa kuzingatia wana mipango ya kutaka kutwaa ubingwa kwa msimu huu. Timu inayotaka ubingwa inatakiwa kuwa na mwendo wa ushindi bila ya kujali imecheza vibaya, vizuri au inacheza na mpinzani wa aina gani.

 

Kwa mwendo huu nadhani ipo haja ya kutulia na kutafuta wapi pa kufanyia kazi kwa ajili ya kurudi kwenye hali yao ya ushindi na kuonyesha ukubwa wao. Yanga wanatakiwa kukila kidonge kichungu ili wapate unafuu wa ugonjwa wao na kuacha kukipaka asali kila siku.

Wakifanya namna hiyo naamini wanaweza kurudi kwenye njia sahihi lakini hili litawezekana kukiwa na misingi mizuri ya kiuongozi, wachezaji na benchi la ufundi kuifanya kazi yao vyema na utulivu wa mashabiki wao.


Lakini ajabu ni kwamba inawezekana Yanga wana vitu viwili lakini wanakosa kimoja kati ya nilivyosema hapo juu. Yanga haina utulivu katika suala la mashabiki wake.

 Mashabiki hawa licha ya kwamba wanaona wanafanya yale yaliyo sahihi kwa ajili ya timu yao lakini niwaambie wazi kwamba ndiyo wanaochangia kwa kiasi kikubwa kuivuruga timu yao na kuipeleka kwenye njia ambayo siyo sahihi.

 

Inajulikana wazi shabiki ni mchezaji wa 12 lakini kucheza kwa mashabiki wa Yanga kumezidi kwa sababu unaona wakati ambao wanatakiwa kukaa kwa kutulia na kusaka suluhu ya matatizo yao wao wamelipuka na kuja na suala la kuhujumiwa kwa timu yao.

 Ninachojiuliza kwenye dunia hii ya utandawazi hiyo hujuma ambayo wanaisema ni ipi na nani ambaye anaifanya na wao wamejiridhisha kwa kiwango gani kiasi kwamba wakaja na jibu kwamba sare mfululizo ambazo zinajitokeza kwa wakati huu zinatokana na hicho ambacho wanafanyiwa?


Madrshabiki hao walitangaza kufanya kisomo au dua kwa ajili ya kuwasomea dua watu wote ambao wanaifanyia mabaya timu hiyo lakini cha kujiuliza ni lini walikaa chini na kuwaombea nyota wao waweze kufunga mabao kwenye nafasi ambazo wanazikosa?

 Lingekuwa jambo la msingi na zuri zaidi na lenye busara kama tungesikia kwamba wachezaji wa Yanga wameombewa dua kwa ajili ya kukingwa na mabaya na waweze kufunga mabao kwa sababu hilo ndilo tatizo kubwa ambalo linakisumbua kikosi hicho.

Lakini kwa muda huu ambao watu wanafanya mambo yasiyo na msingi naona dhahiri yanaipotezea muda timu hiyo na yanawaondoa kwenye malengo ambayo wamejiwekea.

 Kitu muhimu zaidi ni kukaa na kutazama wapi tatizo lililpo. Wahenga wanasema ‘mvua inyeshe kuonekane panapovuja’ hiki ndiyo kitu kinachohitajika kwenye klabu hiyo na sio hizi siasa zisizo na maana wanazofanya.

 

 

1 COMMENTS:

  1. Wachezaji wa yanga wamelewa rushwa au uchawi hamna kitu hapo, tujipange mapinduzi cup mwakani ndio level yetu

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic