HESABU ambazo zipo kwa sasa kwa kila timu ni kuona namna gani ambavyo zinaweza kuvuna pointi tatu kwenye mechi zao ambazo watacheza kwa sasa.
Hakuna unyonge kwa timu ambazo zinashuka uwanjani mzunguko
huu wa pili, kila mtu anaonyesha uwezo wake wote kusaka pointi tatu.
KMC walipokutana na Yanga mzunguko wa kwanza ubao ulisoma
KMC 1-2 Yanga na ngoma ilipokuja kuchezwa Uwanja wa Mkapa ilikuwa ni 1-1.
Licha ya kwamba wimbo mkubwa ambao unaimbwa na kila mmoja
kwa upande wa wachezaji pamoja na viongozi ni kwamba waamuzi wamekuwa
hawatabiriki, bado kupata matokeo ni kazi kwa wakati huu.
Hili ni jambo jema kwani ushindani unavyokuwa mkubwa ligi ya
Tanzania inazidi kuwa imara na kufanya bingwa ajaye ajipongeze pale atakapotwaa
taji lake.
Lakini kumekuwa na kasumba ya timu nyingi kuweka mtego
kwamba mechi za mzunguko wa kwanza huwa wanazichukulia kawaida, hakuna yale
mapambano ya kweli yanayoonekana.
Imekuwa kawaida kwamba pale wanapopoteza utasikia bado kuna
mechi zinakuja mbele hivyo tuna nafasi ya kubaki ndani ya ligi.
Hizo mechi ambazo zinakuja zimekuwa zikiwapa presha na
kufanya hata mpira wakitoa wao ukirushwa kwa timu pinzani wapeleke lawama kwa
waamuzi wakidhani wanaonewa.
Sababu ya hayo kutokea ni ile presha ya mchezo, kila mmoja
yupo kwenye presha, wachezaji, benchi la ufundi mpaka mashabiki nao
wanasumbuliwa na presha ya kuona matokeo yanatokea hapohapo.
Hili linapaswa litazamwe kwa ukaribu na timu kiujumla ili
kuweza kupunguza presha ambazo zinaweza kuzuilika mwanzo kabisa wa ligi kwa
hesabu za kuamini kwamba kila mchezo ni muhimu.
Suala la kuamini kwamba kuna mechi mkononi ni ugonjwa ambao
unahitaji tiba. Ili kuweza kupunguza presha ni kuamini kwamba mechi zote ni
fainali na kucheza bila kukamia baadhi ya mechi.
Pia kwa wachezaji wakiwa uwanjani bado ninawakumbusha kwamba
wasitumie presha yao kuwaumiza wachezaji wengine kwa makusudi hili hapana
nasema tena hapana.
Kwa wale mashabiki wenye tabia za kutoa maneno yasiyo mazuri kwa viongozi pamoja na wachezaji
wanapaswa nao wawe na subira na kukubali matokeo ambayo wanayapata.
Imani yangu ni kwamba waamuzi watatembea na zile kanuni zao
17 katika majukumu yao huku wachezaji nao wakicheza , ‘fair play’.
Hii ni lala salama , wachezaji wanatengeneza ugali wao hivyo
ukimtibulia mwenzako utakuwa unataka ashinde njaa, hilo halipendezi, chezeni
mpira kwa juhudi ila faulo zile za kutengeneza acheni.
0 COMMENTS:
Post a Comment