PONGEZI kwa Simba kuweza kufika hatua ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, hapo wamefanya jambo ambalo Tanzania ilikuwa inasubiria litokee na hatimaye limetimia.
Kuongoza kundi A ambalo lina wababe kama Al Ahly, AS Vita na
Al Merrikh sio kitu cha kubeza na wengi wanaweza kuona ni jambo la kawaida hili
ni jambo kubwa mno.
Tunaona kwamba baada ya makundi kupangwa kila mmoja alikuwa
anaitoa Simba na kuiweka nafasi ya tatu kisha Al Ahly ambao ni mabingwa
watetezi pamoja AS Vita walikuwa wanapewa nafasi kusonga mbele.
Kweli walikuwa na haki ya kufikiria hivyo kwa sababu mpira
ni mchezo ambao una matokeo matatu, kushinda, kushindwa na sare kwa kuwa wengi
waliiweka fungu la kukosa Simba mambo yamebadilika.
Bado wapo ambao wanaibeza kwa nafasi ambayo imefika hili
naona sio sawa, Watanzania lazima tujivunie jambo letu katika mashindano haya
ya Kimataifa hakuna haja ya kuwabeza.
Kazi kubwa wameifanya na wametinga hatua ya robo fainali
kuna faida kubwa inakuja kwa kuwa timu zinaweza kuongezeka katika ushiriki wa
Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa.
Kupeleka timu nne ikiwa itakuwa rasmi ni heshima na inakuwa inaonyesha ukubwa wa
Tanzania kwenye ulimwengu wa soka na itazidi kuimbwa na kuheshimwa kwa ukubwa wa
mambo ambayo Simba imefanya.
Wawakilishi wetu pia Namungo FC wao wana kazi ya kujenga
timu ili wakati ujao ifanye vizuri pale itakapopata nafasi kuipeperusha bendera
ya Tanzania.
Mchezo wa kwanza ilipoteza ugenini kwa kufungwa na Raja
Casablanca na ilipokutana na Pyramids ikapoteza pia pointi tatu muhimu.
Kupigwa nje ndani mbele ya Nkana FC ni somo kwa Namungo
pamoja na timu nyingine ambazo zinaweza kupata nafasi kwenye mashindano ya
kimataifa.
Wachezaji wanaonekana kukata tamaa kutokana na matokeo
ambayo wanapata ila wana kazi ya kuendelea kupambana wapate pointi inawezekana.
Nimeona pia benchi la ufundi limekuwa likiweka wazi kwamba
hakuna wachezaji wenye uzoefu hili nalo lichukuliwe kuwa somo kwa timu zetu
kuwa na wachezaji wenye uzoefu.
Jambo kubwa la kufanya ni kukubali kujifunza na pale ambapo
mnakosea mna kazi ya kurekebishana wenyewe kwa wenyewe ili kusaka matokeo
kwenye mechi zenu ambazo mtacheza. Ni wakati wa Namungo kuijenga timu yao ili
iweze kumaliza mechi zilizobaki kwa heshima.
Kila mchezaji anapenda kuona timu inapata matokeo mazuri.
Ikiwa morali itakuwa kubwa kwa kila mchezaji itaongeza nguvu pia ya kupata
matokeo mazuri wakati ujao.
Bado kazi ni nzito ila itarahisishwa ikiwa kila mchezaji
atakubali kujitoa na kutimiza majukumu yake kwenye mechi ambazo watakuwa
wanacheza.
Imani yangu ni kwamba ikiwa wachezaji mtakubali kupambana
kwa ajili ya mechi zote za ushindani kitaifa na kimataifa matokeo mtayapata.
Kikubwa ni kuongeza juhudi bila kukata tamaa.
Kwenye ligi ya Tanzania kwa sasa ni lala salama ambapo kila
timu inapambana na hali yake kuona namna gani inaweza kutimiza malengo ambayo
iliyaweka mwanzo wa msimu na sasa unakwenda kumeguka.
Ushindani kwa timu uwanjani ni mkubwa. Pia kila timu
imewekeza kiasi cha kutosha ikihitaji kupata matokeo, Jambo la msingi ni kwamba
kusiwe na yale mambo ya upangaji wa matokeo kwenye kusaka pointi tatu.
Ni muda wa wachezaji kufanya vizuri ili kuzipa timu zao
matokeo chanya. Hilo litawafanya wazidi kukuza thamani zao sokoni.
Kelele zimekuwa zikizidi kwamba waamuzi wanachezesha chini
ya kiwango huku zile sheria 17 zikionekana kupindishwa, hili nina amini
litafanyiwa kazi.
0 COMMENTS:
Post a Comment