KUELEKEA mchezo wa marudiano dhidi ya Kaizer Chiefs utakaopigwa kesho Jumamosi, kocha Mkuu wa kikosi cha klabu ya Simba, Didier Gomes amefunguka kuwa amelazimika kutazama tena mara mbili rekodi ya mchezo uliopita ambayo ni sawa na dakika 180, ili kujua nini wanatakiwa kufanya ili kupindua matokeo yao ya kwanza.
Simba Jumamosi iliyopita wakicheza ugenini katika uwanja wa FNB (Soccer City), katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika walikumbana na kipigo cha mabao 4-0 ambayo yameweka rehani nafasi yao ya kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.
Simba inatakiwa kushinda mchezo wa kesho Jumamosi kwa tofauti ya mabao 5-0 ili kufufua matumaini yao ya kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.
Akiwazungumzia wapinzani wake, Gomes amesema: “Tulipata nafasi ya kuangalia mapungufu yetu, nami binafsi niliutazama mchezo ule mara mbili, hivyo tayari tumefanyia marekebisho matatizo yetu.
"Naamini kama hatutarudia makosa na tukajitoa kwa uwezo wetu wote bila shaka hakuna kinachoshindikana, na tunajiamini kuwa tunayo nafasi kubwa ya kuweza kupindua matokeo.
“Sijui nini kitatokea Jumamosi (kesho), lakini najua
tutashinda na tutatumia mbinu za tofauti kabisa kumaliza mchezo.”
0 COMMENTS:
Post a Comment