May 13, 2021


SUALA zima la uahilishaji wa mechi ya watani wa jadi kati ya Simba na Yanga ambayo ilipaswa kuchezwa Mei 8, Uwanja wa Mkapa bado imekuwa na mambo mengi ambayo yanawachanganya wadau pamoja na mashabiki.

Ipo wazi kwamba kila mmoja kwa sasa anahitaji kujua hatma ya mchezo huo utachezwa lini ila ni jambo ambalo linahitaji subira kwa kuwa mamlaka husika zimeweza kuliweka sawa suala hili kwa kueleza kuwa tarehe itatajwa.

Wengi walikuja ili kuona na wengine walikuwa wamekuja kutoka nje ya mkoa wa Dar ipo wazi na wengine walikuja kutoka nje ya mipaka ya ardhi ya Tanzania.

Kweli unapozungumzia mchezo wa Simba dhidi ya Yanga ni aina ya mchezo ambao ukubwa wake ni gumzo kila kona hivyo kuyeyuka kwake bado ni gumzo kila kona kwa sasa kwa kuwa hakuna ambaye alitarajia kwamba itatokea hivyo.

Mashabiki wengi walihitaji kupata burudani na wengine walitarajia kutazama burudani wakiwa nyumbani kwa sababu mpira ni burudani na ni furaha pia hasa watani wakiwa wanakutana.

Ninapenda kuzipa pongezi mamlaka za ulinzi na usalama kwa namna ambavyo waliweza kuimarisha kazi kazi zao na kutimiziza majukumu yao katika wakati ule mgumu.

Pia mashabiki wanastahili pongezi kwa utulivu kwa sababu sio jambo jepesi zaidi ya mashabiki buku kutoka salama kwa utulivu ule licha ya purukushani za hapa na pale.

Unajua unapozungumzia mashabiki kujitokeza uwanjani halafu kile ambacho walikitarajia wakakikosa huwa kunakuwa na mambo mengi ya kufikiria, lakini yote kwa yote ilikuwa ni busara za mashabiki kuweza kuelewa namna kizungumkuti kilivyokuwa.

Kwa namna yoyote ile pole na pongezi ziwafikie mashabiki na wakati huu bado wanapaswa kuendelea kuwa watulivu wakati mamlaka zikiendelea kufanyia kazi yale ambayo yalitokea ili haki itendeke.

Haijawahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni na kwa karne ya sasa ya uwazi na ukweli inakuwa ni ngumu kuweza kuamini kwamba imetokea katika ardhi ya Tanzania ila hakuna namna tayari jambo limeshatokea.

Kwa kila upande kulikuwa na mkanganyiko wa mambo jambo ambalo limefanya mambo yawe kama yalivyo kwa sasa hamna namna ni suala la kusubiri na kuona ni kitu gani kitatokea.

Vyombo husika vifanye mambo ambayo yatasimamia haki bila ya upendeleo kwa kuwa tumeona kwamba kila sekta imekuwa inatoa tamko lake yote ni sawa ila iwe ni katika kusimamia haki.

Tunaona kwamba suala hili limetinga mpaka bungeni ambapo limejadiliwa. Hii inaonyesha kwamba suala hili sio jambo dogo na ni muhimu kulitazama kwa ukaribu na kwa umakini zaidi.


Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) imani yangu ni kwamba linatambua kwamba kwa sasa lina kazi ya kuweka usawa na kufuata haki katika hili kwa sababu kila kitu kinaendeshwa kwa mujibu wa utaratibu ambao umewekwa.

Tukumbuke kwamba kwa sasa tupo kwenye lala salama timu  na kila timu zinapambana na hali kuona namna gani zinaweza kupata matokeo.

Ipo wazi kwa zile ambao zitakuwa zimejiandaa ni muhimu kutambua kwamba zitapata kile ambacho zinastahili jambo ambalo ni ushindi uwanjani.

Kwa zile ambazo zitashindwa kujipanga vizuri basi zijiandae kushuka daraja kwani hakuna jambo jingine ambalo watalivuna kwa wakati huu.

Pia hata Ligi Daraja la Kwanza ni lala salama tunaona kwamba Mei 15 ni timu mbili ambazo zinapambana kuona namna gani zinaweza kupata ushindi kwenye mechi hizo.

Geita na Pamba hizi kwenye kundi lao nafasi zao za kupanda kwenye ligi zinategemea mechi zao za mwisho ambazo watacheza hivyo yule ambaye atashinda atapanda Ligi Kuu Bara jumlajumla, atakayepoteza hapo safari ya kucheza play offs inaweza kumsubiri.

Ikumbukwe kwamba Geita wanaongoza kundi na wananafasi ya kupenya ikiwa tu watapata sare huku ndugu zao Pamba wakipoteza ama kupata sare. Na Pamba wakishinda, Geita wakapata sare safari ya Ligi Kuu Bara inakuwa ni ya Pamba hivyo ni aina ya mchezo ambao ni wa hesabu nyingi.

Hapa sasa mamlaka husika zina kazi ya kufanya kazi kwa weledi na kutimiza sheria pamoja na kanuni ili baadaye kusiwe na vilio vingine wakati ujao kwa kuwa lawama zimekuwa ni wimbo ambao hauna tiba.

Zipo ambazo zinapambana kwenye kushuka daraja ipo wazi kwamba maisha ya Ligi Daraja la Kwanza yanahitaji nguvu nyingi na akili katika utendaji.

Mfano mzuri ni Alliance, Mbao FC, Singida United hizi zilikuwa zinacheza ndani ya ligi msimu uliopita ila kwa sasa hazina uhakika wa kubaki ndani ya Ligi Daraja la Kwanza.

Singida United wao wameshashushwa madaraja mawili kwa kuwa walikwama kupeleka timu uwanjani hivyo hawa wana safari nyingine ya kurudi Ligi Kuu Bara.

Kazi kubwa kwa wachezaji iwe kutafuta ushindi katika mechi zao zijazo na kupambana kwa hali na mali kupata wanachostahili.

 Mbeya Kwanza wao washakamilisha kazi yao na wataanza maisha mapya msimu ujao ndani ya Ligi Kuu Bara msimu ujao. Huku kazi ni moja kusaka pointi tatu kwenye kila mechi.

Wasisahau zile jitihada ambazo walizitumia kupanda ligi basi huku pia wanapaswa kuziendeleza kwa nguvu na kasi zaidi.

2 COMMENTS:

  1. Tumechoka sasa kusikia habari ya mchezo wa SIMBA na Yanga ambao tayari Serikali na vyombo vinavyo simamia mpira vimekwisha liweka sawa jambo hili. Tunataka kusikia mambo mapya na yenye afya kwa mpira wetu. Ramadhan Kareem

    ReplyDelete
  2. Maana kila kukicha na Simba na Yanga kana kwamba hakuna timu zingine

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic