June 17, 2021

 


IPO wazi kwamba timu nne zinakwenda kushuka ndani ya Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wa 2020/21 na kufanya zaidi ya wachezaji 100 kutokuwa kwenye mfumo msimu ujao kutokana na sababu mbalimbali.


Ikumbukwe kwamba ulikuwa ni mpango mrefu wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) katika kupunguza idadi ya timu ambapo kwa sasa zipo 18 na msimu ujao zinatakiwa kuwa 16.


Kwenye kila faida inapotokea na hasara itakuwepo pia kwani hakuna ambaye atanufaika bila kuumia na kwa wakati huu ninaona kwamba hasara ambayo inakwenda kupatikana ni kubwa.


Kwa kuwa ni timu nne zitashuka maana yake ni kwamba nguvu kazi ya wale wachezaji inakwenda kupotea jumlajumla na haijulikani wapi itakwenda kuwa.


Zile ambazo zitashuka kwenda Ligi Daraja la Kwanza kumekuwa na tatizo kubwa la wale wachezaji waliokuwa na timu hizo kukata tamaa pale ambapo watakosa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara ama watakapopunguziwa maslahi yao.


Ikiwa wanakwenda kuanza maisha mapya hapo inaleta picha kwamba kwa kila timu ambayo ilikuwa imeajiri wachezaji zaidi ya 20 maana yake ni kwamba kuna wachezaji wanakwenda kukosa kazi na kuwa wasaka kazi upya.


Kwa familia ya michezo ni hasara namba moja katika hili ninaona kwamba ni muhimu kukawa na mpango kazi mapema ambao utatumika kuokoa hasara hii inayokwenda kutokea.


Haina maana kwamba nahitaji timu zisishuke hapana, hilo lipo wazi tangu awali ilikuwa inajulikana na ni lazima itokee pale msimu utakapokamilika nne zitashuka.


Imani yangu ni kwamba kwa kuwa TFF wanajua suala hili basi watakuwa wameandaa mazingira rafiki kwa msimu ujao ndani ya Ligi Daraja la Kwanza ili wanafamilia watakapokuwa huko wasijihisi wanyonge.


Kwa kuwaandalia mazingira mazuri hasa katika ligi yenyewe kwa kuwaboreshea mazingira hasa kwa kuanza na kutafuta wadhamini licha ya kwamba ni jukumu la timu na TFF ina mkono wake mkubwa kwa kuwa hawa ni wasimamizi itaongeza nguvu kwao.


Kwa zile ambazo zinakwenda huko Ligi Daraja la Kwanza kutoka huku ndani ya Ligi Kuu Bara ni lazima zijipange kusaka ushindi ili kuweza kurejea wakati ujao ndani ya ligi.


Kikubwa kinachohitajika ni maandalizi makini na kila mmoja kutimiza majukumu yake kwa wakati sahihi jambo litaongeza ushindani na kuleta matokeo mazuri.


Ikiwa zitakuwa huko Ligi Daraja la Kwanza zinapaswa kufanya maandalizi mazuri kwenye kila mechi ili kupata matokeo chanya na hatimaye kuweza kurejea ndani ya ligi tena.


Lakini itapendeza pia mazingira ya utendaji kazi huku Ligi Daraja la Kwanza yakaboreshwa na kuwa yenye ushindani mkubwa kuondoa zile lawama ambazo zimekuwa zikiimbwa kila siku.


Rai yangu ni kuona kwamba hawa wachezaji zaidi ya 100 ambao wanatoka kwenye ligi wayakute mazingira mazuri yatakayowafanya wasifikirie kufanya jambo lingine kwa kujiweka kando na masuala ya soka.


Imekuwa hivyo hata kwa zile ambazo zilishuka wakati uliopita kuna wachezaji wengi ambao walikuwa na uwezo mkubwa baada ya kuona kwamba wanashiriki Ligi Daraja la Kwanza waliamua kujiweka kando na kwa sasa hawapo kwenye ulimwengu wa mpira.


 Hapo kikubwa ni kuona kwamba muda ujao hawa wachezaji ambao ni hazina ya taifa wanaendelea kubaki kwenye soka na hata wakati ujao watakaporudi kwenye ligi waendelee kupambana.


Imani yangu ni kwamba zile ambazo zimepanda zinatambua kwamba kuna ushindani mkubwa kwenye ligi na wanatambua pia kuna suala la kushuka na kurudi kule ambapo wametoka.


Wanachotakiwa kufanya ni maandalizi hakuna jambo lingine ambalo litawafanya waweze kuwa bora katika mechi ambazo watacheza kwa msimu ujao katika maisha yao mapya.


Kwa wachezaji wanapaswa kutambua nidhamu ni suala la lazima kwao ikiwa wanahitaji kufikia mafanikio yao kila wakati katika soka.


Itawafanya waweze kuwa bora muda wote ndani ya uwanja na kuyafikia mafanikio yao hilo ni suala la kuzingatia na kuliweka katika akili zao.


Ipo wazi kwamba msimu ujao utakuwa na ushindani mkubwa tofauti na msimu huu ambao nao umechangamka kwa timu kusaka ushindi.


Jambo la msingi ni kuona kwamba hawa wachezaji ambao wanaondoka ndani ya ligi wanalindwa na kuandaliwa mazingira mazuri kwa wakati ujao. 


 


 



1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic