UONGOZI wa KMC umeweka wazi kwamba jambo ambalo wanalihitaji kwa msimu wa 2020/21 ni kumaliza katika nafasi ya nne iliyo mikononi mwa Biashara United.
Ikiwa imecheza jumla ya mechi 29 imekusanya pointi 41 nafasi yake ni ya tano huku Biashara United ipo nafasi ya nne na pointi 45 baada ya kucheza mechi 30.
Akizungumza na Saleh Jembe, Ofisa Habari wa KMC, Christina Mwagala amesema kuwa wanahitaji kumaliza katika nafasi ya nne hilo ni jambo ambalo lipo wazi.
“Wachezaji wanajua na uongozi unajua mpaka benchi la ufundi, sasa hapo kazi ni moja ligi itakaporudi kupambana kupata pointi tatu na kumaliza ligi nafasi ya nne na maandalizi yapo vizuri.
"Ushindani ni mkubwa na kwa sasa tayari tumeanza maandalizi ukizingatia kwamba kuna muda mrefu ambao tutakaa bila mechi.
"Ambacho tutakifanya ni kucheza mechi za kirafiki pamoja na kuendelea kujiandaa zaidi kwani malengo lazima yatimie na inawezekana," amesema Mwagala.
Mchezo wao ujao wa ligi ni dhidi ya Dodoma Jiji unatarajiwa kuchezwa Juni 17, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
0 COMMENTS:
Post a Comment