June 26, 2021


 KOCHA wa Simba, Didier Gomes ameichimba mkwara Azam FC kuelekea kwenye mchezo wao wa nusu fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Azam unaotarajiwa kupigwa leo kwenye Uwanja wa Majimaji mkoani Songea.

 

Mchezo huo wa kihistoria ambao ni muhimu kwa timu kupata ushindi ili ifuzu hatua ya fainali ambayo bingwa atakata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika, mwakani.


Timu hizo katika mchezo wa mwisho kukutana kwenye Ligi Kuu Bara ni Februari 7, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam uliomalizika kwa sare ya kufungana mabao 2-2.

 

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes, amesema kuwa maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na kikubwa wanataka kufuzu kucheza fainali.

 

Gomes amesema kuwa malengo yao katika msimu huu ni kutetea mataji yote wanayoyashikilia kwa kuanzia ligi na Kombe la FA, hivyo ni lazima wawafunge wapinzani wao Azam.


“Lazima tuonyeshe tunataka kufika fainali kwa kujituma na kuonyesha uwezo.Lazima tuchukue ubingwa wa ligi na lazima tuchukue FA.


 “Tunawaheshimu Azam FC, ni timu kubwa na ngumu ambayo tulikutana nayo katika ligi, lakini licha ya ukubwa wao lazima tuwafunge ili tucheze fainali,” amesema Gomes.

 

Kwa upande wa nahodha wa timu hiyo, John Bocco, amesema kuwa: “Tunaenda kukutana na timu nzuri, tunawaheshimu kwa hilo lakini tumejipanga vizuri na Mungu atatusaidia kupata matokeo mazuri na kufuzu fainali.”


Mshindi wa mchezo wa leo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Majimaji atakutana na Yanga iliyokata tiketi ya kutinga hatua ya fainali.


Yanga ilipenya hatua hiyo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya  Biashara United ya Mara.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic