KWA miaka minne sasa kwenye benchi la wachezaji wa akiba wa Yanga kuna jina la golikipa Ramadhani Kabwili, hii ni baada ya kipa huyo kupandishwa kwenye kikosi cha timu ya wakubwa ya klabu hiyo.
Kabwili alipandishwa kikosi cha
wakubwa baada ya kuonyesha uwezo mzuri akiwa na timu ya Serengeti boys
ilichoshiriki kwa mafanikio michuano ya kombe la mataifa ya Afrika (AFCON), kwa
vijana yaliyofanyika nchini Gabon mwaka 2017.
Kabwili anaonekana kuwa kipa wa
kawaida sana kwa kuwa tu anasugua benchi pale Yanga, lakini nikukumbushe kuwa
huyu ni miongoni mwa walinda mlango wazawa ambao wana vipaji vikubwa vya soka.
Aliweza kulithibitisha hili
katika ‘dream team’ ile ya Serengeti boys iliyofanya makubwa katika michuano ya
kombe la mataifa ya Afrika kwa vijana mwaka 2017.
Unaweza kujiuliza inawezekanaje
kipaji kama cha Kabwili kikaendelea kupotelea benchi? Kama ishu ni uzoefu hiyo
haiwezi kuwa hoja yenye nguvu kubwa kwani tayari amefanikiwa kucheza michuano mikubwa
ikiwemo michuano ya AFCON ya mwaka 2017.
Lakini amewahi kucheza michezo
mikubwa ya Ligi Kuu Bara ikiwemo mchezo wa dabi ya Kariakoo uliopigwa Februari
16, 2019 ambapo Simba walishinda kwa bao 1-0, huku Kabwili akifanikiwa
kuonyesha uwezo mkubwa.
Nafasi ya mlinda mlango ndani ya
Yanga imekuwa na changamoto kubwa kiasi kwamba mpaka sasa wakiwa wamecheza
michezo 31, tayari wameruhusu kufungwa mabao 21, manne kati ya hayo wakifungwa
katika michezo miwili iliyopita ambapo kwa nyakati tofauti makipa, Metacha
Mnata na Faroukh Shikalo walisimama langoni.
Hali hii imekuwa ikiwakera si tu
mashabiki wa Yanga lakini hata wachezaji na viongozi wa klabu hiyo ambao mara
kwa mara wameonyesha hasira zao za wazi, na hata kufikia pointi ya kuanza
kuangalia uwezekano wa kusajili kipa mpya.
Ni wazi kuwa mpaka sasa Yanga ni
miongoni mwa klabu tatu ambazo tayari zimejihakikishia nafasi ya kucheza
michuano ya kimataifa kwa msimu ujao, ambapo Tanzania inatarajia kupeleka timu
nne katika mashindano hayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na yale ya kombe la
Shirikisho.
Hivyo ni wazi Yanga wanapaswa
kufanya jitihada za ziada kumaliza tatizo hili kabla ya kuanza vibarua vya
michuano hiyo ya kimataifa, kwa kuwa katika michuano hiyo kuna nyota wengi wa
viwango vya juu na kama ni kweli wanataka kushindana na si kushiriki hawana
budi kumaliza changamoto kwa kufanya usajili katika maeneo yote ambayo
yanaonekana kuwa na mapungufu.
Ni kweli listi ya makipa wa Yanga
inahusisha makipa wengi bora, lakini kuelekea michuano hii ya kimataifa unatakiwa
kuwa na makipa wa kiwango cha juu zaidi.
Yanga ni lazima waachane na angalau kipa mmoja, na kusajili kipa mwingine mwenye uwezo mkubwa zaidi na uzoefu wa kucheza michuano ya kimataifa.
Lakini pia litakuwa jambo la
busara zaidi kumpa nafasi Kabwili ambaye nina uhakika amejifunza mbinu za
kutosha, na kilichobaki kwa sasa ni ishu ya kumpa nafasi ya kuthibitisha ubora
wake uwanjani, na siyo kusubiri mpaka tutengeneze 'hashtag' ya Kabwili.
Uchambuzi wa Vuvuzela unaokujia kila siku ya Jumatano ndani ya gazeti la Championi.
Acha kuizungumzia Yanga tafuta lingine ongelea mikia wenzio hata Kama Ana kaa benchi hiyo haikuhusu
ReplyDelete