MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’, mapema Jumatano aliwaandalia chakula cha mchana wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi la timu hiyo, ikiwa ni muda mfupi kabla ya kuelekea Kigoma kucheza dhidi ya Yanga.
Mo Dewji alikutana na mastaa wa Simba na kuzungumza nao mambo mbalimbali ikiwemo mikakati ya kuelekea mchezo huo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam utakaochezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Tukio hilo lilifanyika katika kambi ya timu hiyo iliyopo Kunduchi, Dar es Salaam.
Pia Mo Dewji alitumia fursa hiyo kuwapongeza mastaa wa timu hiyo na viongozi wa benchi la ufundi baada ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2020/21.
Chanzo cha uhakika kutoka katika kambi hiyo, kimeliambia Spoti Xtra kwamba, Jumatano Sikukuu ya Idd, viongozi wa benchi la ufundi na wachezaji wa Simba walipata mualiko huo kutoka kwa bosi wao huyo.
"Mo ameandaa sherehe ya kuwapongeza wachezaji na benchi la ufundi kwa kitendo cha kutwaa ubingwa wa ligi, pia kuna mikakati inawekwa kwa ajili ya kwenda kufanya vizuri dhidi ya Yanga katika mchezo wa fainali ili tutetee tena kombe lingine msimu huu,” kilisema chanzo hicho.
Mkuu wa Maudhui wa Simba, Ally Shatry ‘Chico’, ameliambia Spoti Xtra kwamba, baada ya maandalizi ya takribani siku mbili, kikosi cha timu hiyo Alhamisi jioni kilielekea Kigoma tayari kuikabili Yanga.
“Kuhusu maandalizi yote kwa ajili ya mchezo yamefanyika,” alisema Chico.
0 COMMENTS:
Post a Comment