KLABU ya Yanga inaelezwa kuwa imemalizana na nyota wa kikosi cha Dodoma Jiji, Dickson Ambundo kwa dili la miaka miwili.
Jana wakati Yanga ikikamilisha hesabu za mzunguko wa pili kwa msimu wa 2020/21 ilicheza na Dodoma Jiji jambo ambalo liliwapa nafasi mabosi wa timu hiyo kuonana na kiraka huyo.
Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ulisoma Dodoma Jiji 0-0 Yanga jambo ambalo liliwafanya wagawane pointi mojamoja.
Kwenye msimamo, Yanga ipo nafasi ya pili na pointi zake ni 74 huku Dodoma Jiji ikiwa nafasi ya 8 na pointi zake ni 44.
Awali Ambundo alikuwa anatajwa kuingia kwenye rada za Simba baada ya Kocha Mkuu, Didier Gomes kuweka wazi kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wanafanya vizuri uwanjani ni pamoja na Ambundo ambaye anavaa jezi namba 7.
Aliyasema hayo jijini Dar baada ya Simba kucheza na Dodoma Jiji, Uwanja wa Mkapa.
Taarifa kutoka kwa mtu wa karibu wa Ambundo zimeeleza kuwa nyota huyo amekubali kutua Yanga na kwa sasa kinachosubiriwa ni muda na kukamilisha makubaliano.
"Ambundo yupo tayari kutua Yanga na tayari kuna mambo ambayo wameyakamilisha atajiunga hivi karibuni kwa dili la miaka miwili ikiwa mambo yote yatakuwa sawa," ilieleza taarifa hiyo.
Kuhusu usajili kwa sasa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa bado dirisha la usajili halijafika hivyo wakati ukifika kila kitu kitakuwa wazi.
0 COMMENTS:
Post a Comment