KATIKA moja ya vitu ambavyo Waafrika tumebarikiwa na tunapaswa kujivunia ni kuwa na vipaji halisi vya usakataji kabumbu.
Ukiangalia katika mitaa mbalimbali ya uswahilini katika nchi zetu za Afrika, hautochoka kuangalia vijana mbalimbali wakisakata mpira wa makaratasi huku wakionyesha vipaji vya soka.
Ni ukweli usiopingika maeneo hayo ambayo yanajulikana kama uswahilini, ndio hayo hayo yanayotoa wachezaji wengi wenye vipaji vya hali ya juu ambao makuzi yao kwa asilimia kubwa yanakuwa yanategemea zaidi soka.
Maisha magumu na kipato cha chini cha walio wengi, bado si kikwazo cha kuficha na kutoonyesha vipaji vyao walivyopewa na Mungu kupitia miguu yao.
Hapa Tanzania pia ukiangalia asilimia kubwa ya vijana wanaosakata kabumbu wanatokea katika mazingira ya uswahilini huku wengi wakitegemea soka hilo hilo kuendeshea maisha yao ya kila siku.
Lakini, bahati mbaya vijana wengi wenye vipaji, wanaishia kupotea kwa kucheza michezo ya ndondo mpaka umri unapowatupa mkono, kutokana na kukosa muelekeo na njia sahihi ya kufikia malengo yao.
Ni asilimia ndogo waliobahatika kidogo kupita katika njia sahihi angalau wameweza kupenya katika timu mbalimbali zikiwemo zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini nao ukiwatazama kwa jicho la tatu utabaini hawakuandaliwa vya kutosha.
Kitu cha kusikitisha ni mfumo mbovu wa utawala wa soka ambao umekuwa kikwazo cha kuweza kuwasaidia au kuwajengea njia sahihi wachezaji hao kuweza kufikia malengo yao, tangu hatua za awali za usakataji wa gozi la ng’ombe.
Hebu leo tupia macho kikosi cha timu ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 23 ambayo imefanikiwa kubeba ubingwa wa Cecafa ambapo michuano hiyo ambayo ilikuwa ikifanyika nchini Ethiopia.
Tanzania inayonolewa na Kocha Kim Poulsen, imetwaa ubingwa huo baada ya kufunga Burundi kwa penalti 6-5 kufuatia suluhu ndani ya dakika 90.
Vijana hao wameonesha kuimarika na kuonesha hali ya matumaini kwa soka letu kwa siku zijazo kwa jinsi wanavyocheza.
Lakini vijana hao wanatukumbusha kikosi cha umri wa miaka 17, ambacho kiliweza kufanya vizuri na kunyakua ubingwa wa dunia nchini Afrika Kusini lakini leo tukiwatafuta hao vijana hatufahamu hata walipopotelea.
Leo tunahangaika kufanya majaribio ya wachezaji wa kuchezea timu ya taifa kila kukicha wakati tayari tulishavuna wachezaji ambao wangekuwa ni hazina tosha kwa taifa letu katika michuano mbalimbali ya kimataifa.
Uzuri ni kuwa vijana wengi wako tayari na timu zao ambazo zinashiriki ligi kuu na madaraja mengine hivyo ni vyema wakaendelea kutunzwa kwani tayari wameonyesha njia nzuri ambayo wameanza kuionyesha na kitendo cha kutwaa ubingwa huo na kuzishinda timu za taifa ambazo huwa tunaziona bora kuliko sisi ni hatua kubwa.
Timu zilizoshiriki ni Uganda, Tanzania, DR Congo, Burundi, Ethiopia, Eritrea, Kenya, Sudan Kusini na Djibouti hizi zote hakuna hata ya kubeza moja na utaona vijana walipambana na wakafanikiwa kuwashinda wote hao.
0 COMMENTS:
Post a Comment