MSHAMBULIAJI wa Yanga, Heritier Makambo, amefunguka kuwa baada ya kufanikiwa kuwavua Simba ubingwa wa Ngao ya Jamii, sasa mipango yao ni kuhakikisha wanawavua tena ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Jumamosi iliyopita katika mchezo wa Kariakoo Dabi kuwania Ngao ya Jamii uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba. Taji hilo lilikuwa likishikiliwa na Simba.
Akizungumza na Spoti Xtra, Makambo alisema: “Kwanza kabisa kama wachezaji tumefurahishwa sana na matokeo ya mchezo wetu dhidi ya Simba, ushindi lilikuwa jambo muhimu kwa kuwa tulikuwa tumetoka kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Jambo zuri ni kuwa tumeshinda ubingwa wetu wa kwanza na sasa macho yetu yote ni kuhakikisha tunaanza vizuri kwenye ligi baada ya kumaliza kazi yetu mbele ya Simba kwa kuwa tumeshatwaa Ngao ya Jamii.
“Nina furaha kuwa tumeanza vizuri kwa kuwafunga watani wetu, kwetu huu ni mwanzo mzuri na nina imani tutazidi kufanya vizuri, huu ni mwaka wetu, tunawaahidi mashabiki kupambana kwa ajili yao.”
Ikumbukwe kuwa, Simba ndiyo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara wakibeba ubingwa huo mara nne mfululizo kuanzia msimu wa 2017/2018 hadi 2020/21.
Makambo jana Septemba 29 alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao walicheza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2021/22 ambapo Yanga ilishinda kwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar.
Mtupiaji wa bao alikuwa ni mzawa Feisal Salum aliyemtungua kipa wa Kagera Sugar, Chalamanda.
0 COMMENTS:
Post a Comment