JUMAPILI iliyopita ilikuwa ni kilele cha Wiki ya Mwananchi ambapo kikosi cha Yanga kilishuka dimbani kuvaana na Zanaco FC kwenye mchezo wa kirafiki ambao Yanga ilikubali kipigo cha mabao 2-1 na kufanya sherehe hiyo kumalizika vibaya kwa mashabiki na wanachama wa timu hiyo.
Zanaco ilikuwa ni kipimo sahihi kwa Yanga ambayo haikuwa na maandalizi bora ya msimu hadi sasa huku kukiwa na ingizo jipya la wachezaji wengi ambao wanahitaji muda kuweza kufahamiana na kutengeneza muunganiko mzuri na wenzao ndani ya kikosi.
Yanga hawakuwa na muda mzuri wa kufanya maandalizi ya msimu kwani kambi yao kule nchini Morocco haikuchukua hata wiki moja na waliamua kuvunja na kuja kujiandaa na msimu mpya nchini.
Hivyo walitumia muda mwingi safarini kuliko uwanjani.Ikumbukwe kuwa mwezi huu Yanga itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Rivers United kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Yanga inahitaji kupata matokeo ili iweze kuvuka hatua inayofuata.
Kipigo walichokipata Yanga dhidi ya Zanaco kiwaamshe kutoka kwenye usingizi wa Wiki ya Mwananchi na waanze kufanya maandalizi thabiti kujiandaa na michuano ya kimataifa kwani kwenye hatua za awali ya michuano ya kimataifa iwe Shirikisho au Ligi ya Mabingwa ni mechi ambazo zimejikita zaidi kwenye mahesabu makubwa kuliko kitu chochote.
Wanapaswa kutambua kuwa kwenye michuano kimataifa unapaswa kuzitumia nafasi kila zinapopatikana na hupaswi kufanya makosa ya kizembe kwani muda wowote unaweza kuadhibiwa kwa aina ya makosa ambayo utayafanya.
Ni michuano ambayo kila timu inakuwa makini na inapambana kuhakikisha inatengeneza nafasi nyingi kadri wanavyoweza na kuzitumia kwa ukubwa wake.Benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu Mohammed Nabi huu ndiyo muda wa kuanza kufanya maboresho makubwa ndani ya kikosi kwa kuhakikisha anatengeneza timu ya ushindani ambayo itaweza kupambana kwenye kila mchezo ambao watashuka dimbani.
Msimu wa mashindano haupo mbali ni takribani wiki moja imesalia kabla ya michuano ya kimataifa kuanza kutimu vumbi na Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Shirikisho la Azam lipo njiani kuanza kutimua vumbi hivyo ni lazima maandalizi yafanyike mapema.
Ukikiangalia kikosi cha Yanga kimejaa wachezaji wazuri na wenye vipaji vya hali ya juu lakini kinachokosekana hivi sasa ndani ya kikosi hicho ni timu kutokuwa na muunganiko mzuri kutokana na kutopata muda wa kutosha kufanya maandalizi.
Ni lazima muutumie muda huu kufanya maboresho kikosini ili msimu unapoanza msijikite kwenye kutafuta vizingizio zaidi kuliko kutafuta matokeo uwanjani, kwani mnapokuwa na vikosi imara lawama ambazo hazina msingi kwa marefa na Bodi ya Ligi nina imani hayatakuwepo.
NA BONIFACE PAWASA
0 COMMENTS:
Post a Comment