SELEMAN Matola, Kocha Msaidizi wa Simba SC, amewatuliza Wanasimba kisha akasema: “Msimu wa 2021/22, tutafanya vizuri katika mashindano yote.”
Msimu uliopita, Simba ilibeba Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam, huku ikifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kikosi cha Simba ambacho kiliweka kambi nchini Morocco kwa takribani siku 17, juzi Jumamosi kilirejea rasmi Dar baada ya kukamilisha kambi yao hiyo.
Simba wakiwa njiani kurudi Tanzania kutokea Morocco, walikutana na baadhi ya wale wa Yanga ambao nao walikuwa wakirudi Dar wakitokea kambini Morocco.
Kwa pamoja wakatua Dar.Awali baadhi ya wachezaji wa Simba na Yanga waliondoka huko Morocco baada ya wengine kuitwa kwenye timu zao za taifa, huku Yanga ikimaliza kambi yao Jumapili iliyopita.
Akizungumza na Spoti Xtra, Matola alisema wachezaji waliopo ndani ya kikosi wana ushirikiano mkubwa pamoja na sapoti ambayo wanaipata kutoka kwenye uongozi ni moja ya sababu zinazowapa nguvu ya kufanya vizuri.
“Kila baada ya msimu kuisha huwa kunakuwa na mpango kazi na kwa hesabu ambazo tunazo tunaona kwamba bado tuna nafasi ya kufanya vizuri msimu ujao ambao utakuwa na ushindani mkubwa.
“Kikubwa ambacho tunakiona ni upekee na uwepo wa nyota wenye uzoefu katika kikosi chetu. Hakuna namna ambayo tunaweza kusema kwa sasa zaidi ya kuwaomba mashabiki waendelee na utamaduni wao wa kuwa pamoja nasi bega kwa bega,” alisema Matola.
Katika kipindi ambacho kikosi cha Simba kilikuwa kambini Morocco, kilicheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya FAR Rabat na Olympique Club de Khouribga ambayo yote iliisha kwa ya sare.
Kaimu Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema: “Baada ya kukamilisha kambi yetu ya takribani wiki tatu nchini Morocco, kikosi rasmi kinarudi Dar ambapo kitakuwa na mapumziko mafupi kabla ya kujiandaa na kambi yetu ya pili.
“Kambi ya Morocco imekuwa ya mafanikio makubwa sana kwetu kupitia programu za mazoezi, lakini pia michezo miwili ya kimataifa ya kirafiki ambayo tulifanikiwa kucheza," .
0 COMMENTS:
Post a Comment