KAMPUNI ya kimataifa ya mchezo wa kubashiri, 10bet imezindua rasmi shughuli zake barani Afrika ikiwa ni pamoja na Tanzania, katika malengo yao ya kuendeleza mpira wa miguu ambapo mpaka sasa timu kutoka mataifa sita zitaanza kufaidika na udhamini wa kampuni hiyo.
Miongoni mwa timu hizo ni Dodoma Jiji FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Mbali ya timu ya Dodoma Jiji, timu nyingine ni Talanta ya Kenya, Enyimba (Nigeria), Aduana Stars (Ghana), Red Arrows (Zambia) na DC Motema Pembe ya DR Congo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya 10bet Africa, Arthur Perry amesema kuwa wameamua kuingiza shughuli zao katika bara la Afrika, ili kuleta maendeleo ya kweli ya mpira wa miguu na timu hizo sita zitaingia makubaliano ya miaka mitatu kila moja.
Perry amesema kuwa kampuni yao inajisikia fahari sana kuingia udhamini na timu za Afrika kwa lengo ni kuleta maendeleo.
“Tumehamasika sana kuingia katika makubaliano na ushirikiano wa klabu hizi. Lengo ni kuleta maendeleo ya kweli katika mpira wa miguu Tanzania na Afrika kwa ujumla.
“Ni hatua kubwa katika kuelekea lengo ambalo tumejiwekea ikiwa ni kuwapa furaha mashabiki wa mpira wa miguu duniani kote.
“Huu ni mwanzo tu, tumedhamiria kufanya mambo mengi ya kimaendeleo katika mpira wa miguu kupitia michezo yetu wa kubashiri," amesema Perry.
Ameongeza kuwa wameanza kuendeleza vipaji katika nchi mbalimbali, ikiwa lengo kuu ni kuibua wachezaji mastaa kama Mbwana Samatta na Samuel Chukwueze wa Nigeria.
Alifafanua kuwa wachezaji wengi chipukizi wanashindwa kufikia malengo yao kutokana na ukosefu wa vifaa vya kufundishia na kampuni yao pia imeanza zoezi la kusaidia eneo hilo na pia kusaidia mafunzo ya makocha.
0 COMMENTS:
Post a Comment