BAADA ya kutofunga bao lolote kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes amemkingia kifua mshambuliaji wa kikosi hicho, Chriss Mugalu na kusema kuwa ni jambo la kawaida mshambuliaji kushindwa kufunga.
Simba ilipoteza mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, Septemba 25.
Baada ya mchezo huo kumalizika, mashabiki wengi wa Simba walimlaumu mshambuliaji wa timu hiyo, Mugalu baada ya kukosa nafasi ambazo zingeleta mabao ambayo mashabiki hao waliamini huenda wangepata ushindi kwenye mchezo huo.
Chanzo cha ndani ya Simba kimeliambia Championi Jumatano kuwa: “Baada ya mashabiki kutoa lawama nyingi kwa mshambuliaji wetu Mugalu, Kocha Gomes amesema kuwa jambo hilo ni la kawaida kwa mshambuliaji kukosa mabao, hivyo ataendelea kumtumia katika michezo mbalimbali.
“Gomes ameonekana kuvutiwa na kiwango cha Mugalu licha ya malalamiko hayo kwani anatekeleza maelekezo yake na akiwa katika eneo la ushambuliaji anawasumbua sana mabeki wa timu pinzani kitu ambacho anaelekezwa na kocha mazoezini.”
Kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United, Mugalu hakucheza na ni Meddie Kagere na John Bocco walikuwa na jukumu la kuongoza safu ya ushambuliaji.
Katika mchezo huo timu hizo ziligawana pointi mojamoja na Biashara United waliweza kupewa mkwanja mrefu ambao ni milioni 10 kutokana na kupata sare hiyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment