Mwanasoka mkongwe wa zamani, Patrick Yondani amesema kuna
kila dalili msimu ujao mkoa maarufu nchini kwa masuala ya soka, Mwanza utakosa
timu inayoshiriki Ligi Kuu Bara.
Yondani ambaye ni baba mzazi wa beki nyota wa Yanga na Taifa
Stars, Kelvin Yondani alisema ubinafsi na watu kutopendana miongoni mwa wadau
wa soka, limekuwa ni tatizo.
Lakini serikali ya mkoa wa Mwanza imeshindwa kung’amua mapema
kuhusu umuhimu wa Toto African mapema na umeamua kuibuka sasa.
“Ukiangalia kwa sasa ni sawa na tumechelewa, kama juhudi
zingeanza mapema na serikali ya mkoa ilikuwa ina kila sababu ya kuijali Toto.
“Toto ndiyo inatusaidia kuziona timu za ligi, lakini wengi wa
wadau wa soka hapa Mwanza hatupendani na badala yake tuna mapenzi zaidi ya
Yanga na Simba kuliko hata Toto ambayo tungeweza kuisaidia.
“Lakini hata watu wanaofanya kazi za Toto wametanguliza sana
ushabiki wa baadhi ya timu za Dar es Salaam, mwisho inakuwa tatizo,” alisema
Yondani.
Enzi akiwa mwanasoka Yondani alikuwa akicheza kama
mshambuliaji na Mwanza ilikuwa ina timu kadhaa zinazotamba ikiwemo Pamba
maarufu kama TP Lindanda.
0 COMMENTS:
Post a Comment