Siku chache baada ya mambo kuanza kwenda mlama
na viongozi kadhaa kuanza kujiuzulu, hali ya hofu na kuhujumiwa imeanza kutanda
ndani ya Simba.
Inaonekana mambo si mazuri kwa maana kuna watu
ambao ni mashabiki au wadau wa klabu hiyo wameanza hujuma za chinichini ili
kuipoteza Simba njia.
Mmoja wa viongozi wa Simba, hakutaka kutajwa
ameeleza kuwa wako katika uchunguzi ili kubaini nyendo za wanaowahujumu
kutokana na hofu waliyoanza kuipata.
“Kweli tuna hofu, huenda mambo si mazuri na
kuna viongozi walio madarakani au waliojiuzulu hawataki maendeleo ya klabu. Inawezekana
wako wanaotaka kuonyesha kuondoka kwao kutasababisha Simba isiwe na amani.
“Simba ina watu wengi sana, inaweza kwenda
bila ya mtu mmoja. Sasa hatuwezi kusema ni nani, lakini lazima tufanye
uchunguzi kuangalia inakuwaje.
“Kuna taarifa tumeletewa, kwamba kuna mmoja wa
viongozi wa zamani wa Simba ameanza kuhujumu na ana urafiki na wachezaji wetu. Sasa
hili ni tatizo, lakini siku ya mwisho tutabaini, ndiyo maana hatuwezi kutaja
majina,” alisema kiongozi huyo.
Lakini mdau mwingine wa Simba, amesema moja ya
hofu kubwa kwamba kuna hujuma, ni wachezaji wakongwe kuwa na sababu nyingi siku
chache kabla ya mechi ya Coastal Union.
“Wachezaji wakongwe walianza taratibu
kujiondoa kwenye timu na kutoa sababu ambazo siku ya mwisho zilisababisha timu
iwe na vijana tu. Lakini tukacheza na kushinda.
“Lakini utaona pia, timu kabla haijaenda
uwanjani tukazuiliwa pale hotelini, Dhaira, Mudde na Basena nao wakatimuliwa
hotelini. Kama mwepesi kung’amua, jiulize kwa nini mambo haya yanayotekea sasa.
“Kweli hili jambo linashangaza, lakini ni
picha inayoonyesha kiasi gani viongozi wetu wanavyokuwa watu wanaojifikiria wao
tu bila ya kujali wengine. Hawataki Simba ifanye vizuri, kisa wao hawapo. Ni kitu
kibaya sana na kinazidi kuwafunua wasivyo waaminifu.
“Sisi tunajua, katika wale ambao hawako Simba
leo, kiongozi mmoja wa zamani ameanza kuwa tatizo. Tutafanya kila tunachoweza
kumkamata, hatuwezi kukubali kudhalilishwa au kuharibiwa mambo kwa kuwa tu eti
yeye hayupo.”
0 COMMENTS:
Post a Comment