Wachezaji wa Simba waliokwama mjini Mwanza wanatarajia
kuondoka jijini humo leo saa saba mchana kwenda Bukoba.
Kiungo nyota, Amri Kiemba amesema tayari wameelezwa hali ni
nzuri mjini Bukoba na ndege zinaweza kutua.
“Tumeanza kujiandaa, nafikiri saa sita tutakuwa airport kwa
ajili ya safari ya kwenda Bukoba, tumeambiwa mambo yote safi na ndege zinaweza
kutua Bukoba,” alisema Kiemba.
Wachezaji waliokwama Mwanza ni wale waliokuwa katika kikosi
cha timu ya taifa, Taifa Stars iliyokuwa vitani kupambana na Morocco na
kufanikiwa kuishinda kwa mabao 3-1.
Wachezaji hao ni Kiemba, Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Nassor
Said ‘Chollo’, Mrisho Ngassa na Mwinyi Kazimoto ambaye aliachwa jijini Dar.
Walitarajiwa kuwasili Bukoba jana mchana, lakini mvua kubwa
zilizonyesha mjini humo zilisababisha uwanja wa ndege kujaa maji na ndege
kushindwa kutua.
0 COMMENTS:
Post a Comment