Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewataka
viongozi wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa kuhakikisha wanaingiza wachezaji
wenye umri sahihi katika michuano ya U15 FIFA Copa Coca-Cola 2013.
Ametoa
mwito huo leo (Machi 26 mwaka huu) wakati akifungua semina elekezi ya michuano
ya Copa Coca-Cola ambayo kuanzia mwaka huu itakuwa ikishirikisha watoto wenye
umri chini ya miaka 15.
Rais
Tenga amesema hakuna jambo la kipuuzi kama kuchomekea wachezaji ambao wamezidi
umri unaotakiwa kwa vile lengo la michuano ya aina hiyo ni kubaini vipaji na
kuwafanya watoto wapende kucheza mpira wa miguu.
“Kwanza
nawashukuru kwa kutenga muda wenu na kuhudhuria semina. Lakini ni vizuri pia
mkahakikisha mnakuwepo kwenye mashindano ili kutekeleza haya ambayo
tutakubaliana katika semina hii. Mkileta mtu mwingine anaweza kutuanzishia
mambo mengine badala ya yale tutakayokubaliana,” amesema Tenga.
Pia
ameishukuru kampuni ya Coca-Cola ambaye imekuwa ikidhamini michuano hiyo tangu
mwaka 2007 ambapo semina hiyo elekezi inayoshirikisha makatibu wa vyama vya
mpira wa miguu vya mikoa na waratibu wa mikoa wa michezo ya UMISSETA ni ya saba
mfululizo.
Ratiba
ya michuano hiyo kuanzia mwaka huu imebadilika ambapo sasa itaanzia ngazi ya
wilaya Aprili wakati fainali katika ngazi ya Taifa itachezwa Septemba.
BONIFACE WAMBURA
MSEMAJI TFF
0 COMMENTS:
Post a Comment