Beki wa kushoto wa Yanga, Stephano Mwasyika anatarajia kuanza mazoezi keshokutwa Jumatano.
Mwasyika alikuwa anasumbuliwa na maumivu makali ya ‘kiazi’ cha mguu wa kulia, hali iliyomlazimu apumzike mazoezi kwa muda.
Daktari wa Yanga, Nassor Matuzya amesema tayari Mwasyika ameanza kurejea katika hali nzuri, hivyo anatarajia kuanza mazoezi yake Jumatano.
“Ataanza mazoezi ya taratibu kwa kipindi fulani huku tukiangalia hali yake inaendelea vipi. Kadiri siku zinavyokwenda nitakuwa nikifuatilia hali yake kwa ukaribu zaidi.
“Iwapo afya itakuwa imeimarika, basi mara moja ntamkabidhi kwa mwalimu ili aendelee na mazoezi katika programu zake za kawaida,” alisema daktari huyo mzoefu wa masuala ya michezo.
Mwasyika ni kati ya wachezaji wa Yanga waliokosa takribani mechi tano za timu hiyo na amekuwa akishindwa kushiriki vilivyo na kutoa mchango wake kutokana na kuandamwa na maumivu.
Beki huyo mzoefu alijiunga na Yanga akitokea Prisons ya Mbeya na tokea wakati huo amekuwa tegemeo lakini siku za hivi karibuni amekuwa akipata upinzani mkubwa kutoka kwa Oscar Joshua.
0 COMMENTS:
Post a Comment