Mshambuliaji mwenye kasi wa Simba, Mrisho Ngassa jana alijikuta katika wakati mgumu katika
mazoezi ya timu hiyo.
Simba ilikuwa mazoezini katika Viwanja vya Leaders, Kinondoni
jijini Dar es Salaam na Ngassa alichelewa kufika takribani dakika 10.
Hali hiyo ilimuudhi Kocha Mfaransa, Patrick Liewig ambaye
alimzuia kuanza mazoezi moja kwa moja na kumtaka azungumze na Meneja, Moses
Basena ambaye tayari alionekana kuwa amepata maelekezo ya Mfaransa huyo.
Baada ya mazungumzo yaliyochukua takribani dakika sita,
Ngassa aliruhusiwa kuungana na wenzake. Ila Wakati huo wengine tayari walikuwa
wameanza mazoezi chini ya Liewig na msaidizi wake Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
Ngassa aliwasili uwanjani hapo harakaharaka akiwa kwenye gari
yake aina ya Nissan, alibadili nguo haraka na kutaka kuungana na wenzake, ndipo
mzungu ‘alipokomaa’.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala alikuwa karibu kabisa
akishuhudia Ngassa akibandikwa maswali na Basena kabla ya kuruhusiwa kuingia
uwanjani kuanza mazoezi.
Siku chache zilizopita, Liewig alimtimua mazoezini
mshambuliaji Felix Sunzu ambaye alitoweka katika timu bila ya kusema lolote kwa
siku kadhaa, halafu akarejea na kutaka kuanza tu mazoezi.
0 COMMENTS:
Post a Comment