Kiungo wa pembeni wa Yanga, Nizar Khalfan amelazimika kufanyiwa uchunguzi wa kiafya zaidi katika hosptali ya Mwananyala jijini Dar es Salaam.
Nizar aliumia na kutolewa katika mechi ya Ligi Kuu Bara wakati Yanga ilipoivaa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumamosi.
Katika mechi hiyo, Yanga iliibuka na ushindi wa bao moja lililofungwa na Nizar kabla ya kuumia na kutolewa nje.
Daktari wa Yanga, Nassor Matuzya amethibitisha Nizar kufanyiwa uchunguzi katika hospitali hiyo.
“Kweli hilo limefanyika, lakini hali yake inaendelea vizuri kabisa. Ilikuwa ni lazima tufanye hivyo kwa kuwa Nizar aliumia.
“Tunashukuru hali yake inaendelea vizuri, atakuwa akiendelea na matibabu na akipata nafuu atarejea kazini,” alisema Matuzya.
Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts amekuwa akionekana kumpa nafasi Nizar tofauti na ilivyokuwa awali alipotua na kujiunga na timu hiyo.
Nizar ni kati ya wachezaji waliocheza nje ya Tanzania katika nchi tofauti kama Vietnam, Kuwait, Canada na Marekani kabla ya kurejea nyumbani na kujiunga na Yanga.
0 COMMENTS:
Post a Comment