Rais wa Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) amewataka wadau wa mchezo huo kuwa watulivu
kwa vile tofauti zilizojitokeza kati ya Shirikisho na Serikali zitamalizwa kwa
taratibu za mpira wa miguu.
Amesema nia ya TFF
ni kuhakikisha Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa) haliifungii Tanzania
kwani tayari Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella
Mukangara alishaahidi kuwepo kikao kati yake na viongozi wa TFF
kitakachofanyika Jumanne (Machi 19 mwaka huu).
“Suluhu itapatikana
kwa mazungumzo kati ya Wizara na TFF. Naamini suala hili tutalimaliza baada ya
kikao cha Machi 19 ambacho kimepangwa na Waziri kutokana na maombi ya TFF,”
amesema Rais Tenga na kuongeza kuwa tatizo lilianzia kwenye mchakato wa
uchaguzi ambao umesimamishwa na Fifa.
Fifa ilisimamisha
Mkutano Mkuu wa uchaguzi baada ya baadhi ya wagombea walioenguliwa kulalamika,
na yenyewe kuahidi kutuma ujumbe wa kushughulikia suala hilo.
Rais Tenga amesema
lisingetokea tatizo hilo, TFF tayari ilishaitisha Mkutano Mkuu ambao
ungefuatiwa na uchaguzi. Lakini kwa vile Fifa ndiyo iliyosimamisha mkutano huo,
TFF inalazimika kusubiri hadi Fifa itakaposhughulikia suala hilo na kutoa
maelekezo ikiwemo lini mkutano ufanyike.
Amesema kwa kuamini
tatizo hilo litamalizwa ndani ndiyo maana TFF hadi sasa haijapeleka Fifa
maagizo ya Waziri Dk Fenella ya kutengua marekebisho ya Katiba ya TFF ya mwaka
2012, kuitisha Mkutano Mkuu wa marekebisho ya Katiba na Mkutano Mkuu wa
Uchaguzi, kwani ingefanya hivyo Tanzania ingefungiwa mara moja.
TFF inasisitiza
kuwa Fifa ilijua tatizo la Serikali kutoa maagizo kwake kupitia vyombo vya
habari, hivyo kumuandikia Rais Tenga na kueleza msimamo wake iwapo itabainika
kuwa Serikali imekuwa ikiingilia uendeshaji wa shughuli za mpira wa miguu.
Uhalali wa kuwepo
kwa barua ya Fifa kwenda kwa Rais Tenga juu ya suala hilo ulihojiwa pia na
mwandishi wa Reuters, Brian Homewood baada ya kusoma kupitia vyombo vya habari
nchini kuwa Shirikisho hilo huenda likaifungia Tanzania ikibainika Serikali
inaingilia shughuli za TFF. Mawasiliano kati ya Fifa na mwandishi huyo ambapo
majibu yake pia TFF ilipewa nakala yameambatanishwa katika taarifa hii.
BONIFACE WAMBURA
MSEMAJI TFF
0 COMMENTS:
Post a Comment