April 9, 2013



 
Na Saleh Ally
SIMBA anazidi kudidimia, hali ya ngozi yake, manyoa si bora tena kama ilivyokuwa awali. Lakini hata utembeaji wake unaonekana ni wa kuchechemea na hakuna ubishi baada ya muda huenda myama huyo maarufu katika soka anaweza kukaa kabisa kwa kushindwa kutembea.

Ubabe wa Simba umeyumba, hakuna amani ndani ya tumbo lake na hata macho yanaonyesha ujasiri wake haupo tena. Mwisho wake ni aibu mbabe kama huyo atakaa barabarani.

Hakuna ubishi Simba haiwezi kuwa bingwa, lakini dalili zinaonyesha haiwezi kushika nafasi ya pili kama mwendo ndiyo huo lakini inaweza pia kuingia katika aibu ya kushika nafasi ya nne na ndiyo  “ kukaa njiani”.

Kweli hali ya Simba si nzuri, kuanzia uongozi wa juu, hadi ndani ya kikosi, kila mmoja anaonekana kupigania ‘roho’ yake. Hakuna anayejali matatizo ya timu na klabu tena. Watu hawapendani tena, hawaaminiani na nguvu ya umoja imepotea. 


Matatizo ni mengi ambayo yanaonyesha kuwa kamwe Simba haitarudi katika reli yake, labda uongozi ubadilike, mioyo irudi nyuma na mambo yaanze upya. Angalia matatizo haya.

Wakongwe vitani:
Asilimia kubwa ya wachezaji wakongwe walioipa Simba ubingwa kama Haruna Moshi ‘Boban’.

Ukali wa kocha:
Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Liewig ni kati ya makocha ambao kwa aina yao, inakuwa vigumu kupata mafanikio makubwa hasa katika nchi za Kiafrika kama Tanzania.

Vigumu kusema si kocha mzuri, lakini mfumo wake wa kutaka kuwaendesha wachezaji kwa ‘remote control’ si mzuri. Anakuwa karibu na uwanja, mpira unapoanza kuchezwa, basi moja kwa moja anaanza kufundisha kwa kelele nyingi.

Ingekuwa vizuri akawaacha wachezaji wacheze soka, marekebisho yawe yanakwenda kwa vipindi. Kumbuka Simba wametoka katika mfumo wa Milovan Cirkovic ambaye alikuwa hapigi kelele nyingi na mpira ‘ulipigwa’ ile mbaya.

Angalia kama Ernie Brandts wa Yanga, Abdallah Kibadeni (Kagera Sugar), Mecky Maxime (Mtibwa Sugar) au Stewart Hall wa Azam FC kama wanafanya hivyo. Si lazima Liewig awe na mtindo kama wa makocha hao, lakini lazima asome maisha ya wachezaji wa ukanda huu, miluzi mingi humpoteza mbwa.

Uongozi butu:
Uongozi uliopo umezidi kuwa butu, matatizo ndani ya Simba yameongezeka, mishahara, fedha za mikataba lakini siku zote Mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage aliyejenga ngome ya makoma-ndoo kumtetea hajui lolote.

Rage anaendelea na maisha yake, timu ikipoteza swali lake huwa: “kwani mimi nacheza namba ngapi”. Kiongozi makini anayetaka kuongoza timu hawezi kuzungumza maneno hayo. Ila hiyo ni picha halisi Simba imefika wapi sasa.

Morali:
Kila timu inahitaji morali ili kufanya vizuri, inawezekana ikawa kwa motisha au hata maneno mazuri yanayojenga. Wako watu wenye uwezo wa kutoa maneno hayo, kwa Simba, kipa Juma Kaseja ni kati ya wanaoweza kufanya hivyo.

Lakini sasa hawezi tena kufanya hivyo, yuko Simba kwa kuwa yupo tu. Lakini ukimuangalia si yule wa zamani, kwani mashabiki walishawahi kuonyesha hawamuamini, uongozi pia ulifanya hivyo, gumzo la kuwa Kaseja amechoka na kuletwa kwa kipa Abel Dhaira lakini ajabu! Kaseja aliyeelezwa amechoka ndiye anayeendelea kuwa msaada mkubwa kwa Simba.

Kwa kiasi kikubwa, kipa huyo ameshuka morali sana. Inawezekana kabisa, kupotea kwake kunaipunguzia Simba mambo mengi hasa suala la uhamasishaji. 

Mbele nyuma:
Kujiuzulu kwa Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope kumekuwa na athari kubwa zaidi kwa kuwa bado Rage amebaki naye hakuwa mtendaji.
Kibaya zaidi, badala ya Rage kulifanyia kazi hilo suala, yeye amekuwa akiendelea kupigania ‘roho’ yake ili aendelee kubaki katika nafasi hiyo.

Rage si mpambanaji kwa maana ya usajili, timu kuingiza fedha na ushawishi kwa wachezaji. Sasa hana watu wa namna hiyo, inawezekana vigumu kuwapata kutokana na rekodi yake ilivyo sasa Simba. Maana yake, jahazi linazidi kuteketea.

 Imani hasi:
Kutoaminiana ndani ya Simba kunazidi kupanda, kila mmoja anamuona mwenzake kama adui au tatizo. Mapenzi yanazidi kupungua na ikitokea mchezaji amekosa bao, au kakosea na kufungisha, basi tatizo linachukuliwa kwa uzito mkubwa kuliko ilivyokuwa mwanzo.
Wako ambao wameelekezewa mitutu ya kutoamiwa, wanafanya mazoezi na kucheza huku wakionekana ni wasaliti. Vigumu wakafanya vizuri wakati wanajua hali hiyo.

Makinda:
Uongozi umesema unawategemea makinda, ndiyo wamechukua nafasi ya wale wakongwe waliotupwa kando. Lakini kichekesho hata waliopewa nafasi nao wanadai na wacheza bila ya kuwa na mikataba.

Morali yao iko wapi? Lazima itakuwa chini na zaidi inategemea hamu yao ya kucheza. Lakini kama wangekuwa na mikataba mizuri, wakalipwa madeni yao, hakika wangekuwa chachu ya mabadiliko.

Hakika hakuna kiongozi mwenye ushawishi na ‘akili’ ya haraka kulifanyia kazi hilo kwa kuwa kila mmoja ndani ya Simba kwa sasa ‘anapigania roho yake’.


2 COMMENTS:

  1. Nakupongeza sana mkuu kwani Umekuwa msaada sana kwa timu hii. Unajitahidi sana kuikosoa sana pale unapoona mambo yanaenda mrama, Hongera sana.Kwani hii itaisaidia sana timu hii kujiweka sawa kama watakuwa viongozi makini.
    Wasiwasi wangu kwako ni kwamba nimeshindwa kukuelewa kwamba huwa unaandika kwa mapenzi zaidi au kwa chuki zaidi. Kwa nini umekuwa unaandika habari za kukosoa sana kwa club hii tu. Kati ya CLUB 14 za ligi kuu yenye uongozi mbovu ni simba peke yake, Ubovu huo umekuja baada ya simba kushika nafasi ya nne. Mbona haya hukuyaandika sana mwaka Juzi na mwaka jana mwanzoni wakati simba ipo kwenye hali nzuri uwanjani wakati uongozi ulikuwa ni huu huu wa Rage unaoutukana kila mara. Vipi kuhusu Uongozi wa Toto ambayo kila mwaka unaponea chupuchupu kushuka daraja na wachezaji wake leo hii weanalia njuaa. Hivi ni kweli club za Mtibwa, Coast, Azam, Kagera Sugar hazina haki ya kushika nafasi za juu zaidi simba na yanga. Mbona
    haukusoi uongozi wa timu hizi. Simaanishi kuwa uongozi wa simba hauna kasoro, wasiwasi wangu ni kuwa kalamu yako badala ya kuisaidia simba inaongeza migogoro tu. Umekuwa unashutumu badala ya kushauri tena mbaya zaidi kwa club moja tuu.Why? Kaka nahisi una ajenda ya siri moyoni.
    Nakuomba sana tuvisaidie vilabu vyetu badala ya kuviangamiza.

    ReplyDelete
  2. Hongera kaka kwa makala yako.... ni uhuru wako wa mawazo , ila je ushauri wako ni upi kama kweli unataka kusaidia utatuzi wa matatizo haya. Je nia yako ni ipi, kama umeshindwa kuyafikisha haya mapungufu kwa wahusika? au unadhani kwa kuandika hapa kwenye blog yako ndio yatafanyiwa kazi. Simba ni kweli inamatatizo na mengi yanakuzwa na nyie Wahandishi wa habari, hakuna mizania katika taharifa zenu. zimejaa maneno ya kuwafurahisha washirika wenu kuliko ukweli halisi.Uzuri wewe ulisafiri na timu Oman na ukaja na makali nyingi za kumsifia mwalimu sasa imekuwaje?.HATUWAELEWI.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic