Beki wa zamani wa Derby County, Plymouth na Inter Milan, Taribo West pamoja na kuwa ameishastaafu, ameingia katika kashfa ya kudanganya umri wake wakati akiwa anacheza.
West raia wa Nigeria alidanganya umri wake na hilo lilijulikana baada ya kujiunga na klabu ya Partizan Belgrade aliyojiunga nayo mwaka 2002.
Wakati akijiunga na Partizan Belgrade kutoka Derby County alisema umri wake ni miaka 28, lakini Rais wa zamani wa klabu hiyo, Zarko Zecevic, amesema baadaye waligundua kwamba alikuwa amefanganya umri na sahihi alikuwa na miaka 40.
“Alivyojiunga nasi akasema ana miaka 28, mwanzo hatukugundua lolote, lakini hata baada ya kugundua sikuona kama kuna sababu ya kumbugudhi kwa kuwa alikuwa akicheza vizuri na kutoa mchango mkubwa kwenye timu.
“Tulijua
wakati anakaribia kuondoka, wakati huo alikuwa na miaka 44, yeye alisema
amefikisha 32. Yote yalijulikana baada ya kuumia goti, baadaye akapimwa na
kuonyesha umri huo.
“Mwisho
hatukumsumbua, lakini tuliamua kumuacha ajiunge na Paykan FC ya Iran ambako
alimalizia mpira wake akiwa na umri halali wa miaka 46 bila ya wengi kujua,”
alisema Zecevic.
Nchi za
Afrika Magharibi zimekuwa na kashfa lukuki katika suala la kudanganya umri na
wachezaji wake wengi wamefanikiwa kuzidanganya klabu za Ulaya.
Taribo West alikuwa mmoja wa mabeki visiki katika ligi za Ulaya alizocheza, lakini pia alipokuwa akiichezea timu yake ya taifa ya Super Eagles.
Nigeria
anakotokea West, imekuwa moja ya nchi zenye tatizo kubwa la udanganyifu wa
umri, hata hivi karibuni waliitoa timu ya vijana ya Tanzania baada ya kufungwa
Dar es Salaam na walipokuwa kwao katika mechi ya marudiano, wakabadili timu na
kujaza vijeba.
0 COMMENTS:
Post a Comment