*Mkataba wake
hadharani, apewa gari tena
*Kuwa na
mshahara mkubwa kuliko wote Bara
Na Saleh
Ally
KIUNGO
mwenye kasi, Mrisho Khalfan Ngassa, amerejea Yanga na kusaini mkataba wa miaka
miwili kuichezea tena timu hiyo.
Ngassa
alianza kupata umaarufu mkubwa akiwa na Yanga kabla ya kuondoka na kujiunga na
Azam FC kwa kitita cha jumla ya Sh milioni 98 na kuweka rekodi mpya ya usajili.
Lakini
Ngassa ameamua kusaini tena mkataba wake mpya Yanga wakati akiwa chini ya klabu
ya Simba ambao ni watani wakubwa wa Yanga.
Simba na Yanga
zinakutana Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa
mwisho kufunga msimu, huku Yanga wakiwa wamepania kulipa kisasi cha mabao 5-0.
Mechi hiyo
ndiyo itakuwa ya mwisho kwa Ngassa ambaye mkataba wake umesainiwa bila kuwa na
tarehe, Championi Jumatano limeshuhudia na lina uhakika asilimia mia.
“Mkataba na
Ngassa kila kitu kimekamilika kama unavyoona, hapa tunachosubiri ni kuisha kwa
msimu na mara moja atatua na kuanza kazi Jangwani,” alisema mmoja wa viongozi
ambao huhusika na masuala ya usajili Yanga.
Alipoulizwa
kwa nini mkataba huo ambao una saini ya Ngassa na dole gumba lake hauna tarehe,
alijibu:
“Bado
hatujajua utaratibu wa TFF kama mkataba ukisainiwa kabla ya mwingine kuisha
inakuwaje. Hatutaki kuingia kwenye matatizo na mtu.
“Kitu
kizuri Ngassa baada ya mkataba wake na Azam FC kuisha, sasa ameamua kurudi
nyumbani, nasi tumemkaribisha vizuri.”
Ingawa
mhusika alifanya juhudi za kuficha eneo la malipo ya Ngassa lakini taarifa za
uhakika zinaonyesha atakuwa analipwa dola 2000 (Sh milioni 3.2) kwa mwezi.
Kwa
mshahara, Ngassa atakuwa mchezaji anayelipwa zaidi ya wachezaji wote Ligi Kuu
Bara. Labda kama kuna timu kati ya Yanga, Simba au Azam FC itasajili mwingine
na kumpa zaidi ya hizo.
Kwa misimu
miwili Felix Sunzu amekuwa akiongoza. Analipwa dola 3,500 (Sh milioni 5.6),
Mzambia huyo amemaliza mkataba na Simba, ataondoka. Wakati Ngassa akiwa Azam na
Simba alikuwa anachukua Sh milioni 2 kwa mwezi.
Kuhusiana
na fedha za usajili, kwa kuwa Ngassa ametua Yanga kama mchezaji huru, tayari ameshatanguliziwa
‘kishika uchumba’ cha Sh milioni 10 pamoja na gari aina ya Nissan Trail ambalo
thamani yake inafikia hadi Sh milioni 23.
Ngassa
amekuwa akilitumia gari hilo alilopewa na Yanga baada ya kuuza alilopewa na
Simba aina ya Toyota Verrosa lenye thamani ya Sh milioni 16 kwa hofu ya
kupokonywa na Simba siku atakaposema anakwenda Yanga.
Kuna
taarifa kuwa Ngassa alisaini mkataba mwingine na Simba ambao angeanza
kuutumikia baada ya mechi hiyo ya Jumamosi.
Simba
kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Pope, imetangaza
kwamba Ngassa alisaini mkataba mwingine wa mwaka mmoja, akapewa gari na fedha
Sh milioni 30 na kama anataka kwenda kokote, basi atalazimika kurudisha fedha
hizo.
Lakini
Ngassa amekuwa akisisitiza hana mkataba na Simba na baada ya huo wa Azam FC
iliyompeleka Simba kwa mkopo utakapomalizika, atakuwa huru kwenda anakotaka.
Ngassa
ambaye yuko kambini na Simba mjini Zanzibar, amewahi kuliambia Championi kwamba
kama Simba inamtaka abaki, basi lazima itoe kitita cha Sh milioni 150.
0 COMMENTS:
Post a Comment