Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall ametia
ruhusa kwa wachezaji wote wageni kurudi makwao.
Wachezaji wa kigeni wanaokipiga Azam
FC ni Kipre Tchetche aliyeibuka mfungaji bora, ndugu yake Bolou Tchetche, wote
raia wa Ivory Coast.
Wengine ni Humprey Mieno, Jockins
Atudo (wote Kenya) na Bryan Umonyi
kutoka Uganda.
Hall raia wa Uingereza ameamua
kuwatumia wachezaji wazalendo tu katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara ambayo
watacheza dhidi ya JKT Oljoro wakiwa ugenini jijini Arusha, Jumamosi.
Uamuzi wa Hall umelenga kuwapa nafasi
wachezaji wazalendo hasa wale ambao hawakupata nafasi.
“Tunaweza kuwatumia wazalendo katika
mechi hiyo, tunajua tukishinda au kupoteza tutabaki katika nafasi ya pili.
“Lakini bado tunauchukulia mchezo huo
kwa ukubwa kwa kuwa pointi zitatufanya tusiwe na pengo kubwa dhidi ya Yanga.
“Tunawaamini wachezaji wazalendo na
nimewapa nafasi hivyo ni vizuri wakaitumia,” alisema.
Msemaji wa Azam FC, Jaffar Idd
Maganga alisema baadhi ya wachezaji wageni walishaanza kuondoka nchini mara
moja baada ya kupata ruhusa hiyo ya Hall.
0 COMMENTS:
Post a Comment