Msanii mahiri wa kizazi kipya Hamis Mwinjuma maarufu
kama Mwana FA ambae ni Balozi wa Chapa Vodacom amesema hadhi na heshima ya
mwanaume katika jamii itakuwa na uzito mbele ya uso wa jamii kwa wao kuwa
tayari kutafuta suluhu ya changamoto zinazoikabili jamii na wala si vinginevyo.
Balozi huyo maarufu kwa jina la
Mwana FA ametoa kauli hiyo mjini Dodoma wakati wa kampeni ya kuelimisha jamii
kuhusu fistula iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square kuelekea siku ya
fistula dunaini Mei 23.
Kampeni hiyo inadhaminiwa na kampuni ya Vodacom na
Vodafone ya Uingereza ikiihusisha mikoa mbalimbali.
Balozi huyo amesema ni wazi kwamba
wanaume wamekuwa wamiliki wa maamuzi katika jamii huku wakitajwa kuwa nguzo ya
familia lakini sifa hizo na mamlaka hayo yatakuwa na dosari kubwa iwapo
hawatokuwa pia mstari wa mbele katika kuhakikisha jamii inapata suluhisho la
matatizo.
Balozi huyo ambae alikuwa
akielimisha wakazi wa mji wa Dodoma kuhusu fistula, amesema fistula sio tatizo
kama ambavyo inaweza kufikiriwa kwa kuwa jambo gumu lingekuwa namna ya kupata
matibabu na uwezo wa kugharamia matibabu hayo.
“Hakuna mwanamke ambaye anapata fistula bila ya
mwanaume kuwa chanzo kwa kuwa ndio tunaowapa ujauzito wake zetu, hivyo sio vema
na haki kwa mwanaume kumkimbia mkewe au kumtenga mwanamke eti tu kwa sababu
mwanamke huyo ana tatizo la fistula,” alisema balozi huyo.
“Nawaomba sana wakazi wa
Dodoma hasa wanaume tubadili mtazamo tulinao juu ya fistula kwa kutambua kwamba
sisi ndio chanzo cha wanawake kupata fistula lakini zaidi ni kwamba hilo sio
tatizo kwa kuwa tatizo ni lile ambalo halina suluhisho, fistula inatibika na
tena inatibika bila malipo kwa ufadhili wa Vodacom na Vodafone, nini zaidi
tunachohitaji katika hili?” alihoji Mwana FA.
Amesema uamuzi alioufanya kukubali
kutembea nchi nzima kuhamasisha akina baba kuondokana na dhana hasi juu ya
fistula ikiwemo kuhusisha tatizo hilo na ushirikina au laana na hivyo
kuwakimbia wake zao au kushiriki kwa namna yoyote katika kuwanyanyapaa wanawake
wenye tatizo la fistula ulikuwa ni mgumu lakini alikubali kwa kuwa anaamini
jamii itamuelewa.
“Haikuwa kazi rahisi kwangu kukubali
kuongoza msafara huu lakini baada ya kutathmini na kuona jinsi akina mama
wanavyoteseka kwa tatizo hili nilijihisi mwepesi kukubali kuzunguka kila kona
kuongea na wanaume wenzangu kuwahamasisha kuwa tayari kwa pamoja kuunga mkono
kampeni hii ili kufikia lengo la Vodacom la kumaliza tatizo la fistula ifikapo
mwaka 2016 .”Aliongeza
“Iwapo kuna mtu(Vodacom)amejitolea
kutoa suluhisho la tatizo kwa kulipia nauli, chakula, malazi na matibabu
hatuwezi tena kusema fistula ni tatizo,kikwazo pekee tulichonayo hapa ni
kuhakikisha kila mmoja anafikiwa na taarifa na ujumbe huu,” aliongeza.
Mwana FA amekuwa chachu katika
kampeni hii kwa namna ambavyo ushawishi wake umewezesha kwa kiasi kikubwa
ujumbe wa fistula kuwaingia wanaume huku baadhi yao wakimuahidi kumuunga mkono
kwa dhati.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Ummy Mwalimu alisema si haki kuendelea
kuwaacha wanawake wakiteseka wakati fursa ya kuwawezesha kupata matibabu ipo na
hivyo ameitaka jamii kuiunga mkono kampeni hiyo na kuitumia ipasavyo.
“Tunaishukuru Vodacom kwa kuweka
mfumo wezeshi kwa jamii kupata elimu ya fistula na pia kuwawezesha wanawake
kupata matibabu ya fistula bila malipo, naomba wakazi wa mji wa Dodoma na nchi
nzima tuitumie fursa hii na tuwe mabalozi kwa wenzetu.”
“Vodacom inafanya kazi kubwa sana
kusaidia jamii hapa nchini. Kamwe hatutoona aibu kuipongeza ndani na nje ya
Bunge kwa kazi hiyo kubwa na znuri wanayoifanya ikiwemo kampeni hii ya fistula
na ufadhili inaotoa kwa wanawake kupata matibabu bila malipo,” alongeza Ummy.
Amesema kuwa jamii lazima ione na
kutambua kuwa mwanamke ana wajibu wa kuwa na afya njema ili nae aweze kushiriki
katika shughuli za kijamii na za kiuchumi na hivyo kuchangia maendeleo ya kaya
na jamii anamoishi.
Naibu Waziri huyo amekiri kuwepo kwa
hali ya unyanyapaa kwa jamii kwa wanawake wanaokabiliwa na matatizo ya fistula
hali ambayo amesema ni lazima ibadilike hasa wakati huu ambapo fursa za
matibabu bila malipo zipo ikiwepo na kuahidi kuibeba ajenda hiyo kwa nguvu zake
zote.
Vodacom hutumia wastani wa Sh
700,000 hadi 900,000 kulipia matibabu ya mgonjwa mmoja wa fistula kwenye
hospitali ya CCBRT.
Nae Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Maendeleo ya Jamii Said Mtanda amesema anatambua vema tatizo la fistula
na athari zake kwa wanawake wazazi na kwamba pamoja na ukweli kuwa amekuwa
akichukua juhudi binafsi katika kusaidia wanawake wenye fistula lakini sasa
anaibeba kampeni hiyo na kuiwasilisha katika kamati yake ili kuipa nguvu rasmi
za kibunge.
“Naahidi kuwa nitawasilsiha kwenye
kamati yangu ujumbe wa kamati hii ikiwa ni pamoja na kuiomba nguvu za kamati
hiyo na kuwashawishi wajumbe kuubeba ujumbe wa kampeni hii ndani ya Bunge
ikiwemo wakati wa shughuli rasmi za kamati na Bunge kwa ujumla,” alisema Mtanda.
Kampeni hiyo iliyolenga kuifikia
mikoa mbalimbali itamaliza safari yake Mei 23 jijini Dar es salaam siku ya
fistula Duniani.
0 COMMENTS:
Post a Comment