Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
limelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuanza upya mchakato wa
uchaguzi baada ya kubaini kasoro iliyotokana na ukosefu wa kutokuwepo vyombo
vya kushughulikia ukiukwaji wa maadili.
FIFA ambayo ilituma ujumbe wake katikati ya mwezi
uliopita kufanya utafiti kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa TFF ambao
ulisimamishwa baada ya baadhi ya wagombea kulalamika, imetaka uchaguzi ufanyike
kabla ya tarehe 30 Oktoba 2013, lakini ukitanguliwa na mabadiliko ya katiba
ambayo yatahusisha uundwaji wa vyombo vya kushughulikia ukiukwaji wa maadili.
Raiswa TFF, Leodegar Tenga aliwaambia waandishi wa
habari kwenye ukumbi wa mikutano wa shirikisho hilo kuwa suala la Tanzania
lilijadiliwa kwenye kikao cha Kamati ya Dharura ya FIFA kilichofanyika tarehe
28 Aprili 2013 na maamuzi yake kutumwa juzi kwa barua iliyosainiwa na
KatibuMkuuwa FIFA, Jerome Valcke.
Baada ya kupokea barua hiyo, Rais wa TFF alifunga
safari kwenda Dodoma jana kukutana na Mheshimiwa Waziri na Naibu wake pamoja na
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
“Matarajio yetu sote yalikuwa kupokea majina ya
waliopitishwa ili tufanye uchaguzi. Kinyume chake tumepokea maagizo hayo. Hata
hivyo tumeona kuwa hili ni jambo la kheri kwa vile siyo tu haki itatendeka bali
pia itaonekana imetendeka.” alisema Tenga, ambaye alishatangaza kuwa hatagombea
tena urais baada ya kuliongoza Shirikisho kwa vipindi viwili vya miaka minne
kila kimoja.
“Lengo letu ni kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa
na uchaguzi kufanyika mapema iwezekanvyo kabla ya tarehe iliyotolewa. Yale
mambo nayoweza kufanyika kwa pamoja yatafanyika ili tuharakishe utekelezaji wa
maagizo yaliyotolewa na FIFA.”
Uchaguzi wa TFF ulipangwa kufanyik tarehe 23 na 24
Februari 2013 na ulikuwa ukielekea ukingoni, lakini baadhi ya wagombea
walienguliwa katika hatua ya mwisho na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na
ndipo walipo andika barua FIFA kuomba iingilie kati.
Rais Tenga alisema kuwa ujumbe wa FIFA ulikutana na
pande zote zilizoathiriwa na mchakato wa uchaguzi na kwamba baada ya kukusanya
taarifa hizo, maagizohayo ya FIFA sasa yatakuwa ni suluhisho la matatizo ya
muda mrefu katika uendeshaji wa mpira wa miguu nchini.
Katika barua hiyo, FIFA imeiagizaTFF:
1. Kuunda vyombo
sahihi (Kamati ya Maadili itakayokuwa na vyombo viwili ambavyo ni cha kutoa
maamuzi ya awali na cha rufaa) ambavyo mamlaka yake yatakuwa ni kushughulikia masuala
ya ukiukwaji wa maadili;
2. Kufanya mabadiliko
ya katiba kwa kuzingatia uundwaji wa vyombo hivyo;
3. Kuanza upya kwa
mchakato wa uchaguzi wa Kamati ya Utendaji kwa kufungua milango kwa wagombea
ambao walishachukua fomu na wagombea wapya:
4. Shughuli hiyo ikamilike ifikapo tarehe 30 Oktoba 2013.
Katika kutekeleza hayo, TFF inatakiwa iitishe Mkutano
Mkuu wa Dharura kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya kuunda
kamati hizo za maadili na Kanuni za Uchaguzi kabla ya kuendelea na Mkutano Mkuu
wa Uchaguzi wa Kamati Mpya ya Utendaji.
Katika maoni yake FIFA imeeleza kuwa katika mchakato,
Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliwaengua au kupitisha baadhi ya wagombea kwa
kubaini kuwa walikiuka Ibara ya 9 (7) ya Kanuni za Uchaguzi na pia Ibaray a 29
(7) ya Katiba ya TFF ambavyo vinahusisha suala la kufungua kesi mahakamani,
kufuja fedha za shirikisho na ukosefu wa uwajibikaji wa pamoja.
Hata hivyo, FIFA ilisema kuwa watu hao walitakiwa
waadhibiwe kwanza na kamati husika (kamati za maadili) kabla ya kuenguliwa na
kamati za uchaguzi za TFF.
“Kutokana na ukosefu wa kamati za maadili matokeo yake,
mmoja wa wagombea amekuwa akienguliwa kwenye uchaguzi kila anapombea bila ya
kujua adhabu yake ni ya muda gani,” inasema barua hiyo ya FIFA.
Rais Tenga ameagiza kuitishwa kwa kikao cha dharura cha
Kamati ya Utendaji ya TFF kupokea maagizo ya FIFA na kupanga ratiba ya
utekelezaji wake kwa lengo la kuhakikisha kuwa mchakato huu unatekelezwa mapema
iwezekanavyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment