Wachezaji wa timu ya vijana ya Simba na wengine wanaoshiriki michuano na programu maalum ya Fels nchini Ujerumani, walipata bahati ya kuzungumza na kupiga picha na Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Loew.
Vijana hao wanaoendelea na mafunzo nchini humo, walitambulishwa kwa kocha huyo ambaye walibadilishana naye mawazo kabla ya kupiga naye picha.
Programu ya Fels inajumuisha mafunzo mbalimbali yanayotolewa na kwa kushirikiana na taasisi ya Mwanza e.V ambayo Mtanzania, Damas Ndumbaro ni mmoja wa viongozi wa Fels.
Akizungumza kutoka Ujerumani, Ndumbaro alisema mafunzo hayo yanaendelea na watoto hao kuzungumza na Loew ni kitu kizuri kama sehemu ya hamasa.
“Sisi kama viongozi pia tulibadilishana naye mawazo, lakini bora zaidi ilikuwa ni kwa watoto hao ambao wamekutana na mtu ambaye ni mwalimu wa wachezaji maarufu duniani,” alisema.
Kikosi hicho cha wachezaji vijana kinaundwa na wachezaji 10, kati yao wakiwemo wanaotokea timu ya vijana ya Simba ambao ni wanne.
Wawili wanaotokea Azam FC waliondoka nchini jana usiku na wameshawasili nchini humo salama na kuungana na wenzao tayari kuendelea na mafunzo hayo.
0 COMMENTS:
Post a Comment