Mtihani wa
uwakala wa wachezaji (players agent) na uwakala wa mechi (match agent) wa
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utafanyika Alhamisi ya
Septemba 26 mwaka huu saa 4 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF).
Kutakuwa na
jumla ya maswali 20 kwenye mtihani huo, 15 yanatoka FIFA kuhusiana na kanuni za
kimataifa za mpira wa miguu na matano yatatoka TFF kuhusiana na kanuni
mbalimbali zinazotawala mchezo huo nchini.
Kwa ambao
wangependa kufanya mtihani huo utakaokuwa katika lugha ya Kiingereza ambayo ni
moja kati ya lugha nne rasmi za FIFA wanatakiwa kujisajili TFF kwa ada ya dola
50 za Marekani ambapo watapewa utaratibu na maeneo ambapo mtihani huo unalenga.
Mtihani huo
utafanyika saa 4 kamili asubuhi, na muda wa kufanya mtihani hautazidi dakika
90.
Mpaka sasa
Tanzania ina mawakala watano wa wachezaji wanaotambuliwa na FIFA. Mawakala hao
ni John Ndumbaro, Mehdi Remtulla, Ally Saleh, Yusuf Bakhresa na Said Tully.
0 COMMENTS:
Post a Comment