Na Saleh Ally, Zurich
NIKO katika programu ya wahariri 18
wanaojifunza mambo muhimu kuhusiana na soka, mengi yanahusisha uendeshaji wa
timu kama kikosi lakini klabu kwa jumla.
Safari yangu imeanzia katika Jiji la
Zurich halafu Basel kabla ya kuingia Ujerumani ambako nitajifunza mambo kadhaa
kuhusiana na vijana wanavyotakiwa kukuzwa na baadaye kuendelezwa vipi.
Nafasi hii ya program ya wahariri 18
wanaojifunza, imetolewa kwa nchi chache sana, Afrika ni nchi nne tu ambazo ni
Ghana, Cameroon, Tunisia na Tanzania ambayo naiwakilisha kama nchi pekee ya
Afrika Mashariki na Kati.
Ziara hii ni ya siku chache tu,
lakini katika siku mbili ndani ya Uswiss, kuna mambo muhimu ambayo nimejifunza
ikiwa ni pamoja na mifumo ya uendeshaji wa ligi lakini namna timu za vijana
zinavyoweza kutumia mamilioni ya fedha na wakati mwingine yasirudi.
Lakini bado watu wanaendelea kuwekeza
bila ya kupata hasara, kitu ambacho ni msaada mkubwa kwa timu zetu za nyumbani
kama wangekuwa tayari kujifunza.
Ndani ya Uswiss, mada kubwa ilikuwa
ni suala la namna ambavyo mifumo inavyoendeshwa, kama unakumbuka Jiji la Zurich
ndipo yalipo makao makuu ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Wao wanaamini ndiyo makao makuu ya
soka duniani, hivyo wanafanya kila linalowezekana kuonekana wanafuata mifumo
husika, moja ni kuendana na kinachoagizwa na Fifa katika uendelezaji wa timu
kupitia mifumo yake.
Hapa Uswiss hakuna soka kubwa
ukilinganisha na England, Hispania au Italia, lakini siku zote wao wanajivunia
kuwa ni sehemu ambayo wachezaji kadhaa wanapitia hapa kwenda kucheza katika
klabu kubwa za Italia, England, Hispania na Ufaransa.
Wanasema nchi nyingi za Ulaya
zinalijua hilo, zimekuwa zikiitumia Uswiss kama sehemu sahihi ya kupata
wachezaji bora uwanjani na nje ya uwanja kwa kuwa makuzi yao yanafuata mifumo
sahihi.
Timu nyingi pia zimekuwa zikifanya
kila linalowezekana ili kuwapeleka wachezaji wao kwa mikopo katika klabu za
nchi hii, kwa kuwa wanatambua watapata mafunzo mazuri na hapo baadaye watakuwa
wachezaji bora katika ligi mbalimbali.
Klabu kubwa maarufu za hapa ni
Grasshopper Club, Basel na FC Zurich, mara chache kuzisikia zinakuwa tishio
katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, ukiacha FC Basel katika siku za hivi karibuni.
Lakini zinakwenda vizuri kutokana na
faida kubwa ya mamilioni ya uero zinazoingiza kutokana na kuuza wachezaji, pia namna
zilivyojijengea mfumo mzuri wa kupata wadhamini ambao wanaziamini kutokana na uendeshaji wao mzuri na wa
kitaalamu usiokuwa na longolongo.
Nilipokuwa nikipata darasa, akili
yangu haraka ikarudi nyumbani ambako tuliamua kuvunja kabisa mfumo wa madaraja.
Kutoka daraja la nne, la tatu, pili, kwanza hadi ligi kuu.
Hakukuwa na sababu kubwa za msingi
ambazo zingeweza kufanya ufafanuzi katika hilo. Utaona kumekuwa na kuyumba
zaidi katika soka ya Tanzania tokea hayo yatokee. Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) wameendelea kuwa wabishi wasiotaka kusilikiza kuhusiana na masuala hayo.
Angalia nchi kama Uswiss ambao
wamepiga hatua wakiwa karibu na kila kitu, lakini wanaona hilo ni bora. Pia
Ujerumani ambao wana hadi ligi daraja la 13, Sweden hadi ligi daraja la saba.
Vipi sisi ambao ni hohehahe tunaendelea kuwa wabishi?
Kama walikosea na wamekubali kuna
tatizo, basi hakuna ujanja wala hakuna haja ya kuona haya, warudishe madaraja
na ikiwezekana hadi daraja la tano ili kuongeza michuano iliyo katika mfumo, na
kupunguza nguvu ya michuano ya mchangani.
Michuano ya mchangani inapata nguvu
sana kwa kuwa hakuna ligi hizo za madaraja, mbaya zaidi mechi za mchangani
hazina faida kimfumo katika soka yetu kwa kuwa zinalenga zaidi burudani tu.
Mfumo unaotumika Uswiss ni kati ya
ile inayotumika katika nchi kadhaa za Ulaya, ligi kuwa na madaraja hadi ya
sita, saba, nane au hata hadi 13 kama ilivyo kwa Ujerumani.
Kutokana na kutokuwa na idadi kubwa
sana ya watu, Uswiss wana ligi hadi daraja la tano, lakini katikati ya Ligi Kuu
na Daraja la Kwanza kuna ligi inaitwa Classic League. Zote zinakwenda katika
mfumo unaofuatana na kila mwaka inafanyika tathmini kama timu zilizopanda au
kushuka zilikuwa zina faida kiasi gani na soka lao.
Tathmini hiyo huwakutanisha wadau
wote, badala ya kuwa na ule mkutano mkuu wa mwaka kwa ajili ya kupiga porojo za
shirikisho, wadau au viongozi wa timu hadi za daraja la tano wanakutana kwa
ajili ya kujadili kilichokuwa bora, wanachotaka kiongezwe au kupunguzwa kabla
ya kuanza kwa msimu mpya.
Kila timu iliyo daraja la juu,
inalazimishwa kwa maana ya kupewa maelekezo ya kuwa na urafiki au usaidizi wa
malezi ya timu za madaraja ya chini kutegemeana na yenyewe itakavyochagua.
Hapa si kutoa fedha, badala yake ni maelekezo
ya mifumo na ikiwezekana kutoa walimu wasaidie timu hizo za chini inapotakiwa.
Ligi ya Uswiss ni ndogo lakini
inaheshimika kutokana na kuwa na mfumo mzuri na uliojengeka kiutekelezaji kwa
asilimia 100. Ndiyo maana nchi kama Liechtenstein ambayo ni jirani yao, imeamua
kuendesha ligi yake ndani ya Ligi ya Uswiss.
Timu saba kutoka Liechtenstein
zinashiriki Ligi Kuu ya Uswiss, nafasi hiyo ya timu saba inabaki kwa timu za
nchi hiyo ambazo zinakuwa zinapambana kupanda na kushuka. Timu za Uswiss pia
huenda kucheza nchini Liechtenstein zikiwa zinaendelea na ligi ya Uswiss.
Ligi ya Uswiss imeweka rekodi ya kuwa
ligi moja inayotumikiwa na nchi mbili na inachezwa katika nchi mbili. Hii
inatokana na mfumo wake kuwa bora na unaoendeshwa kitaalamu na watu wanaotaka
maendeleo ya kweli na si ya kwao binafsi.
0 COMMENTS:
Post a Comment