Aliyekuwa mchezaji kiraka wa Simba,
Shomari Kapombe amejikuta katika wakati mgumu kwa kushindwa kurudi Ufaransa
kutokana na kuchelewa kupata ruhusa ya kuingia nchini humo.
Kapombe anaishi nchini Ufaransa ambako
anaichezea timu ya As Cannes inayoshiriki Ligi Daraja la Nne ‘Sefa’, lakini
ameshindwa kupata visa inayomruhusu kuingia tena nchini humo.
Kapombe alirejea nchini kutokea Ufaransa
kwa ajili ya kuitumikia Taifa Stars katika mechi ya kirafiki dhidi ya Zimbabwe,
hivi karibuni.
Kutokana na hali hiyo, Kapombe amekuwa
akionekana katika mitaa ya Dar es Salaam akiendelea kupambana kupata visa hiyo
itakayomruhusu kurejea tena kazini.
Awali Championi Ijumaa lilikutana na
Kapombe katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na juhudi za kumhoji
kuendelea kuwepo nchini zilikwama baada ya mmoja wa maofisa wa shirikisho hilo,
Saad Kawemba kuzuia kwa juhudi kubwa asizungumze.
Kawemba, huku akiwa amenuna, alimuambia
Kapombe: “Twende twende Kapombe.” Akionyesha kumzuia asihojiwe, naye hakuwa na
ujanja, akatekeleza agizo hilo la kibabe.”
Lakini baadaye, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF,
Boniface Wambura akaonyesha ukomavu na kutoa ushirikiano kwa kuweka mambo wazi
na kusema tatizo la Kapombe ni visa.
“Kapombe yupo hapa nchini kutokana na
visa yake kwisha muda, aliyokuwa nayo ni ya muda mfupi. Ilikuwa inamruhusu
kubaki Ufaransa na akitoka tu, imekwisha na anatakiwa kupata nyingine.
“Kwa sasa haruhusiwi kurejea kule hadi apate
visa mpya, TFF na AS Cannes tumekuwa tukishirikiana ili kumuwezesha kurejea
tena kazini mapema,” alisema Wambura aliyeonyesha ushirikiano.
Tayari Kapombe alipata uhakika wa kuanza
kucheza katika kikosi cha kwanza cha AS Cannes baada ya kurejea akitokea katika
majeruhi.
0 COMMENTS:
Post a Comment