TIMU za Simba na Yanga zimeonyesha kuvimbiana ikiwa ni wiki mbili
kabla ya kuumana katika mechi yao maalum ya promosheni ya Nani Mtani Jembe.
Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Mussa Katabaro amesema timu
yao haina wasiwasi kuelekea kwenye mechi hiyo ambapo mara baada ya kuwakosa
Simba kwa kupata sare ya mabao 3-3, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara, sasa
wataingia na lengo moja kubwa la kutoa kichapo kwenye mchezo huo.
“Hatuna wasiwasi katika mechi hiyo, kikosi chetu kipo sawa na sasa
timu ipo katika mazoezi makali, tunaamini safari hii tutawachapa watani wetu
baada ya kuwakosa katika ligi kwa kupata sare,” alisema Katabaro.
Wakati Katabaro akitamba hivyo, Katibu wa Simba, Evodius Mtawala,
amesema katika kuhakikisha timu yao inafanya vizuri kwenye mechi hiyo, uongozi
wao umeshafanya mabadiliko katika benchi la ufundi kwa kumleta kocha mkuu mpya
Zdravok Logarusic ambapo ujio wake utasaidia kikosi chao kupata ushindi katika
mechi hiyo itakayopigwa Desemba 21, Uwanja wa Taifa jijini Dar.
“Tupo katika kukiandaa kikosi chetu, tayari tumeshabadilisha benchi
letu la ufundi na sasa tuna makocha wapya wakiongozwa na Logarusic,” alisema
Mtawala.
Aidha, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, ambao ndiyo
wadhamini wa timu hizo, amesema kila kitu kipo sawa kuelekea katika mechi hiyo,
ambapo endapo timu yoyote kati ya hizo itaibuka na ushindi, itakuwa ndiyo
zawadi kubwa kwa mashabiki wao kwa kufunga mwaka.
0 COMMENTS:
Post a Comment