Kocha Mkuu wa Simba, Zdravok Logarusic, ameendelea kuwafanyia tathmini
nyota wa kikosi hicho lakini akagundua kuwa ukiacha kipa mpya, Yaw Berko,
hakuna kipa namba mbili na kuagiza atafutwe haraka.
Logarusic ‘Loga’ amesema amewaona makipa wawili mpaka sasa, lakini
Abuu Hashim bado hana ubora wa kuidakia timu hiyo ambapo ameutaka uongozi wa Simba
kumsaka kipa mpya.
“Huwezi kuingia katika vita za kutaka ubingwa ukawa na kipa mdogo kama
yule (Abuu), naomba nieleweke vizuri, siyo kwamba hana kipaji, hapana, katika
eneo hilo yuko sawa lakini anatakiwa kujengwa zaidi taratibu,” alisema Loga.
Kufuatia agizo hilo la Loga, tayari Simba imeanza mchakato huo na
katika kufanikisha jambo hilo, mabosi wa Wekundu hao wamerudi katika mbio za
kumtaka Ivo Mpunda.
“Kama wakiniletea Ivo hakuna shida, huyo ni aina ya kipa ninayemtaka,
nataka mtu mwenye uzoefu mkubwa,” alisema Loga.
Tayari Simba ipo katika mchakato wa kuwasitishia mikataba makipa wao
wawili, Mganda Abel Dhaira na Andrew Ntalla ambao wote wameshindwa kuonyesha
uwezo mkubwa katika mechi za timu hiyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment