Na Saleh Ally
Wakati Luis Suarez akiiadhibu Norwich
City kwa kupiga mabao manne, Liverpool iliposhinda kwa mabao 5-1 na Eden Hazard
akionyesha kiwango cha juu na kushitua wakati Chelsea iliposhinda 4-3 dhidi ya
Sunderland, maswali kibao yakajaa kichwani mwangu.
Hiyo ni hat trick ya tatu ya Suarez
dhidi ya Norwich, yaani kila msimu amefunga mabao matatu kila alipokutana na
timu hiyo bila kujali anacheza ugenini au nyumbani Anfield.
Kwa Hazard kilikuwa ni kiwango cha juu
sana, uwezo aliouonyesha ulimshangaza kila aliyeshuhudia mechi hiyo. Zaidi ya
mara moja mtangazaji alieleza wazi kuhusiana na kiwango cha kushitua cha Hazard
ambaye wakati mwingine aliwachambua mabeki hadi wanne na kutoa pasi murua au
kufunga.
Kufanya vizuri kwa Hazard na Suarez si
kitu kibaya, lakini nilichoangalia ni namna ambavyo wachezaji wageni
wanavyoweza kufanya vizuri England, halafu nikajiuliza kama kweli Tanzania yote
haiwezi kuwa na wachezaji wenye uwezo huo. Ninaamini wapo.
Kama wapo, vipi washindwe kufanya vizuri?
Naamini angalau nusu ya kinachofanywa na washambuliaji hao, inawezekana kufanywa
na wachezaji kutoka Tanzania.
Kwani Watanzania wataendelea
kuwashangilia wengine hadi lini?
Nani anasikia uchungu wa utaifa kwamba kuna
kitu kinaweza kufanyika na mwisho Watanzania wafike mbali na hatimaye kuisaidia
nchi yetu kuendelea kuvikuza na kuvilinda vipaji vinavyokufa bila ya hatia kwa
ajili ya sisi kutokuwa makini au tamaa ya mtu mmoja mmoja?
Unaweza kusingizia malezi ya familia ya
kitajiri kwa akina Suarez na Hazard, lakini jibu ni hapana. Angalia, Hazard hajatokea
katika familia ya kitajiri kwa kuwa baba yake mzazi, Henry na mama yake Carine
wote walikuwa wanasoka.
Baba yake alicheza daraja la pili na
mama yake alikuwa mshambuliaji hatari wa timu ya daraja la pili, aliamua kuacha
soka baada ya kufikisha miezi mitatu ya ujauzito wa Hazard.
Suarez ndiye amekulia maisha ya shida
zaidi kwao Uruguay, hakuwa na malezi mazuri ya familia, maana wazazi wake
walitengana mapema kabisa. Maana yake hawa si matajiri, hivyo suala la fedha au
kutokea familia za kitajiri, tunalifuta.
Tukirudi kwenye mifumo, basi inaonyesha
hivi; wachezaji wanatakiwa kukulia katika malezi mazuri ya soka lakini kingine
muhimu ni wachezaji kuamini kwenye kujituma na kufikia ndoto zao.
Tanzania tuna viongozi wengi wabinafsi,
wanaotaka kuendeleza majina yao, matumbo na familia zao binafsi bila kujali
wanauangamiza kwa kiasi kikubwa mchezo wa soka.
Lakini wachezaji wenyewe pia ni tatizo,
kwamba wengi si waelewa na inaonekana mfumo wa malezi yao kabla ya kufikia leo
kuwa nyota ni tatizo kubwa kwao.
Si waelewa, walalamishi, wavivu na
wasiopenda kujituma. Lakini bado wengi wanaona kucheza Yanga au Simba, ndiyo
mwisho wa safari.
Hakuna ubishi, pamoja na uwezo walionao.
Suarez na Hazard lazima wamefanya kazi ya ziada ikiwa ni pamoja na kujituma
lakini kulenga kufikia ndoto zao ambazo wamekuwa wakitamani kuzifikia tangu
wakiwa watoto.
Viongozi na wachezaji wetu, wengi hawana
ndoto za kufanya kitu fulani na mawazo mengi ni kucheza Ulaya bila ya kuwa na
juhudi zozote.
Ukiangalia vipaji vya watoto na vijana,
kweli ni vingi na vya juu. Lakini mara nyingi wanaishia njiani na hiyo ni picha
tosha kwamba hakuna mfumo mzuri kuanzia katika ngazi za klabu kusaidia kuvikuza
na kuviendeleza vipaji.
Kuna ule msemo wa “kutaka kwenda peponi
kabla ya kufa”. Hili ndilo Watanzania wengi tumekuwa tukilitanguliza. Tunataka
kupata mafanikio makubwa kwa wiki moja, wakati wenzetu wanapambana kwa miaka
ili kuyapata.
Hatupendi kusubiri, hatupendi kukipika
kitu, badala yake tunapendelea kula tu, ikiwezekana bila ya kuivisha. Jiulize,
kuna vijana kweli wanataka kufikia walipo wachezaji hao wa Liverpool na
Chelsea?
Inawezekana wako wachache sana wanaotaka
kufikia kwa akina Hazard na Suarez na uwezo unawaruhusu, kama wakipewa moyo na
kusaidiwa kufika mbele. Lakini nao wamekuwa wakiishia njiani na kukata tamaa kutokana
na kukatishwa tamaa na rundo la lawama bila ya kuwa hata na chembe ya kupewa
moyo.
Wizi wa viongozi wengi kwenye soka pia
ni tatizo. Wanauua mpira pamoja hao vijana. Halafu wanatumia maneno ya ujanja
kuonyesha wao ndiyo wanaonewa na wapo wanaowaunga mkono, mwisho Tanzania
tunabaki kuwa watazamaji na kusifia mazuri ya akina Suarez na Hazard, milele!
0 COMMENTS:
Post a Comment