Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’, leo wametoka suluhu tasa dhidi ya Seeb SC
inayoshiriki ligi kuu ya Oman.
Mechi ya leo ambayo ni ya kirafiki
imeisha kwa matokeo ya 0-0 ambayo inakuwa mechi ya nne tangu kuwasili nchini
hapa Januari 9, kwa ziara ya wiki mbili kujiandaa na ligi mzunguko wa pili
Tanzania Bara.
Coastal Union, imeonyesha uhai katika
kipindi cha pili ambapo kipindi cha kwanza walishindwa kuonyesha makeke yao
baada ya wachezaji wa Seeb, kujazana katikati hali iliyowafanya Wagosi
kushindwa kumiliki mpira.
Aidha, kipa wa Wagosi, Shabani Kado
alipoiona kasoro hiyo akawa anatumia muda mwingi kupiga mipira katikati kila
inapomjia kwa lengo la kuamsha mashambulizi ili viungo wake wachangamke.
Kipindi cha kwanza kiliisha timu zote
kizitoka vichwa chini kutokana na kukosa nafasi za kuonyeshana uwezo
waliofundishwa na walimu wao.
Kipindi cha pili Seeb Club, walifanya
mabadiliko kwa kutoa wachezaji wawili wa ndani na mlinda mlango. Coastal Union
waliendelea kucheza bila kufanya mabadiliko.
Katika dakika za awali kipindi cha pili
Seeb walionyesha uhai na kulisumbua sana lango la Wagosi, lakini kufuli za Juma
Nyoso na Othman Tamim ziliendelea kuwa imara kuulinda mlango wa Shaaban Kado.
Aidha ilipofika dakika ya 76, kocha
Yusuf Chipo alifanya mabadiliko ya haraka haraka kwa kutoa wachezaji wane na
kuingiza wane ndani ya dakika 15 zilizosalia.
Alianza kutoka Othman Tamim akaingia
Abdi Banda, baadae akatoka Danny Lyanga akaingia Mohammed Miraji. Halafu zikiwa
zimesalia dakika chache mchezo kuisha alitoka Atupele Green akaingia Suleiman
Kassim Selembe, halafu akamalizia mabadiliko kwa kumuingiza Abdullah Othman
‘Ustadh’ akatoka Yayo Kato.
Listi ya leo ilikuwa: Shaaban Kado,
Hamadi Juma, Othman Tamim, Juma Said ‘Nyoso’, Mbwana Kibacha, Jerry Santo, Ally
Nassor ‘Ufudu’, Danny Lyanga, Atupele Green, Haruna Moshi ‘Boban’, na Yayo
Kato.
Coastal Union tangu iwasili Oman imeshacheza
mechi nne, imeshinda mechi mbili kati ya Oman Club na Al Mussannah kwa mabao
2-0 kila mechi. Halafu ikafungwa bao 1-0 na Fanja Club, leo imetoka suluhu ya
bila kufungana na Seeb Club.
PICHA: COASTAL UNION
0 COMMENTS:
Post a Comment