Kocha Mkuu
mpya wa Yanga, Hans van Der Pluijm, raia wa Uholanzi, amesema anataka soka la
kasi huku kikosi chake kikicheza kwa ushirikiano katika kushambulia na kukaba.
Van Der
Pluijim (64), amemueleza mmoja wa viongozi wa Yanga kwamba ana imani siku
chache atakazokaa na timu nchini Uturuki, atafanya mabadiliko huku akiahidi
kuwatumia Mrisho Ngassa, Emmanuel Okwi na Simon Msuva katika aina ya ushambuliaji
wa kasi anaoutaka.
“Kocha kasema anapenda soka la kasi,
tumemueleza kuhusu wachezaji kadhaa wenye aina hiyo, amefurahia. Unajua alitaka
kujua baadhi ya mambo, mfano alitaka kujua kama tuna wachezaji wenye kasi,
tumemtajia Ngassa, Okwi, Msuva na amesema pia anataka timu inayocheza kwa
ushirikiano. Lakini naamini ataanza na safu ya ulinzi,” alisema kiongozi huyo.
“Ana mambo
mengi anataka kufanya, lakini ametaka kwanza kuiona timu, vizuri atawaona
wakicheza mechi kwa kuwa atafika kesho (leo), halafu saa chache watacheza mechi.
Atapata nafasi ya kuwaona.”
Kocha huyo
Mholanzi, amekuwa akisifiwa kwa soka la nguvu wakati akiifundisha Berekum
Chelsea ya Ghana na alipofanya mahojiano mafupi na Championi Jumatano,
alisisitiza suala la subira.
SALEHJEMBE:
Unapenda soka la aina gani?
Van Der
Pluijim: Kwanza ni mpira wa kasi, lazima niwe na wachezaji wenye uwezo wa
kumiliki mpira na kupeleka mashambulizi kwa kasi, lakini timu yangu inacheza
pamoja kama timu. Muwe na subira kidogo, lazima wachezaji wajifunze.
SALEHJEMBE:
Labda ulifahamu lolote kuhusu soka la Tanzania?
Van Der
Pluijim: Kwa kusikia ndiyo, ukiangalia timu zinazotoka Tanzania ndiyo maarufu
zaidi kwa Afrika Mashariki, lakini sijui mambo mengi ya hapa.
SALEHJEMBE:
Nini sasa unataka kufanya kwa Yanga?
Van Der Pluijim:
Kikubwa ni kuwa na timu yenye uwezo wa kushinda mechi na baadaye makombe, sina
hofu kwa kuwa Yanga ni timu kubwa.
SALEHJEMBE:
Unajua upinzani wa Yanga na Simba ulivyo?
Van Der
Pluijim: Kokote hilo halikosekani, timu kubwa haikosei kuwa na mpinzani mkubwa.
SALEHJEMBE:
Umewahi kukutana na Logarusic, huyu ni kocha wa Simba. Rekodi zinaonyesha
ulimshinda mabao 4-1, unafikiri itakuwa rahisi kwako kuifunga Simba
mtakapokutana?
Van Der
Pluijim: Ndiyo maana mwanzo nilisema subira inahitajika, Logarusic alikuwa Ashanti
Gold, mimi Berekum Chelsea. Sasa yuko Simba, mimi niko Yanga. Nitalijibu vipi
hilo? Maana sijawahi kuiona Simba anayoifundisha, wala Yanga ninayokwenda
kuifundisha. Halafu tulikuwa Ghana, hapa ni Tanzania, hivyo lazima mambo yaende
kitaalamu kwanza. Vuta subira.
Kocha huyo
alilazimika kuahirisha safari ya kwenda Zanzibar, akapandishwa ndege na kwenda
nchini Rwanda alikopanda ndege kwenda Antalya, Uturuki ambako Yanga imeweka
kambi ya wiki mbili.
Van Der
Pluijm atachukua kikosi hicho wakati Kocha Msaidizi, Charles Boniface Mkwasa
atakuwa anarejea nchini kwa ajili ya sherehe maalum ya ndoa yake iliyotimiza
zaidi ya miaka 20.
0 COMMENTS:
Post a Comment