Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)
imeipiga faini ya jumla ya sh. milioni moja klabu ya Simba kutokana na makosa
mbalimbali ikiwemo vitendo vinavyoashiria ushirikina uwanjani.
Simba ilifanya vitendo hivyo katika
mechi yake dhidi ya Mbeya City ambapo imepigwa faini ya sh. 500,000. Pia
imepigwa faini nyingine ya sh. 500,000 kwa makocha wake Loga, Selemani Matola
na Idd Pazi kuingia uwanjani na kumzonga mwamuzi kwenye mechi hiyo.
Mbeya City imepigwa faini ya sh.
300,000 kwa washabiki wake kuingia uwanjani kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar
iliyochezwa mjini Bukoba. Klabu za Yanga na Coastal Union zimepigwa faini ya
sh. 500,000 kila moja kwa washabiki wao kurusha chupa za maji uwanjani wakati
timu hizo zilipopambana jijini Tanga.
Kiungo wa Mtibwa Sugar, Shabani Nditi
amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga mchezaji wa Simba, wakati Salvatory
Ntebe pia wa Mtibwa Sugar amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumtukana refa
kwenye mechi dhidi ya Mbeya City.
Nayo JKT Ruvu imepigwa faini ya sh.
300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi dhidi ya Simba iliyochezwa
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Vilevile wamiliki wa Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga wameandikiwa barua ya kufanya marekebisho ya vyumba vya
wachezaji, kwa vile havina hewa ya kutosha.
Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) klabu zilizopigwa faini kutokana na makosa mbalimbali ni Friends Rangers
(sh. 200,000), Lipuli (sh. 200,000), Majimaji (sh. 400,000), Polisi Morogoro
(sh. 400,000) na Transit Camp (sh. 200,000).
Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro,
John Tamba atapelekwa kwenye Kamati ya Maadili kutokana na vitendo visivyo vya
kimaadili katika mechi dhidi ya Burkina Faso.
Kiongozi wa Lipuli, Hamis Kiemba na
wachezaji Boniface Sawaka, George Enock na Green Paul watapelekwa katika Kamati
ya Nidhamu kutokana na utovu wa nidhamu waliofanya kwenye mechi dhidi ya
Kimondo.
Naye mchezaji Sangalau Nyamoka wa JKT
Kanembwa aliyelalamikiwa uhalali wake na Polisi Tabora suala lake linapelekwa
Kamati ya Nidhamu.
0 COMMENTS:
Post a Comment