Yanga inatarajiwa kushuka dimbani leo Jumamosi kuivaa Rhino Rangers
katika mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini habari nzuri kwa Wanajangwani hao ni
kuwa, kiungo wao mchezeshaji, Haruna Niyonzima amerejeshwa kundini na yupo
tayari kwa mchezo huo.
Niyonzima alikuwa nje kwa wiki kadhaa tangu alipoanza kuugua malaria
akiwa nchini Misri wakati Yanga ilipoenda kucheza dhidi ya Al Ahly katika Ligi
ya Mabingwa Afrika, ambapo aliikosa mechi hiyo na mbili za ligi kuu dhidi ya
Mtibwa Sugar na Azam FC.
Mechi ya Yanga na Rhino itakuwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi
mkoani Tabora, ambapo daktari wa Yanga, Juma Sufiani amethibitisha kuwa, Niyonzima sasa yuko vizuri kiafya.
“Niyonzima kwa sasa yuko fiti kabisa kuweza kucheza, kinachofuata ni
maamuzi ya mwalimu kumtumia au kutomtumia. Wachezaji
wengine wako fiti kwa ajili ya mchezo huo,” alisema Sufiani.
Aidha, beki wa timu hiyo, Mbuyu Twite, ataendelea
kukosa mchezo huo kutokana na kuwa na matatizo ya kifamilia.
Yanga ina pointi 40, ambazo ni nne nyuma ya vinara Azam, wakati Rhino
inapigana isishuke daraja kwa kuwa ipo mkiani ikiwa na pointi 13.
0 COMMENTS:
Post a Comment