Uamuzi wa Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic raia wa Croatia
kutomtumia kwenye mechi za Ligi Kuu Bara, mshambuliaji Betram Mwombeki
kimewahuzunisha baadhi ya wachezaji wa Simba wakidai kuwa wanahitaji msaada wa
mchezaji huyo uwanjani.
Mwombeki aliyekuwa moja ya wachezaji tegemeo kwenye kikosi cha Simba
katika mzunguko wa kwanza wa ligi kwa sasa amepoteza nafasi hiyo tangu kutua
kwa Loga kwenye mzunguko wa pili wa ligi.
Wachezaji hao ambao hawakutaka kutajwa majina yao gazetini
walizungumza na Championi Jumamosi
kwa hisia kali juu ya suala hilo.
“Yaani sijui hata kwa nini jamaa hatumiki sasa hivi wakati ni msaada
mkubwa sana kwenye mechi zetu, muda mwingine unaona kabisa jinsi gani
anapambana kule mbele akitumia uwezo wake wa ziada aliojaaliwa nao, ila ipo
siku uwezo wa Mwombeki utakubalika tu,” alisema
mchezaji mmoja.
“Kiukweli kabisa hakuna mshambuliaji mpiganaji kama yeye katika hizi
timu za ligi za Bongo, kama kipindi kile alipokuwa anacheza na Amissi Tambwe
kule mbele, yaani mipira ilikuwa inakaa halafu
alikuwa anasaidia kwenye kupiga mashuti,” aliongeza
mwingine.
Loga alikaririwa hivi karibuni akisema kwamba sababu kubwa ya
kutomtumia Mwombeki ni kuumia mara kwa mara kunakomfanya mara nyingi kutokuwa
fiti, hivyo kushindwa kucheza dakika nyingi uwanjani.
SOURCE: CHAMPIONI JUMAMOSI
0 COMMENTS:
Post a Comment