April 7, 2014




Na Saleh Ally
IMEKUWA kawaida kabisa mashabiki kususia timu zao zinapofanya vibaya katika mechi za Ligi Kuu Bara.
Kama Yanga au Simba itapoteza au kupata sare mbili mfululizo, basi idadi ya mashabiki wanaoingia uwanjani inashuka kwa kasi kubwa, hali inayoonyesha ni tofauti kubwa kwenye Ligi Kuu England.

Utaona hali ilivyo katika baadhi ya timu za England kwamba zimeendelea kuingiza idadi kubwa ya watu pamoja na kwamba hazifanyi vizuri.

Manchester United ndiyo timu ‘inayoteseka’ sana katika Premiership kutokana na mwenendo wake kwenye ligi hiyo. Imewahi kukaa nafasi ya saba kwa zaidi ya miezi mitatu, kitu ambacho si kawaida.
Pamoja na hivyo, bado wameendelea kuwa timu yenye mashabiki wengi zaidi wanaoingia uwanjani kwenye Premiership kwa msimu huu.
Manchester United kupitia uwanja wake wa Old Trafford, ndiyo imeingiza mashabiki wengi zaidi ambao ni milioni 1.2.
Kimahesabu, Manchester United, ndiyo timu iliyoshuhudiwa na mashabiki wengi ikiwa nyumbani, ingawa itakuwa na nafasi ya kuonekana kwa mashabiki wengi zaidi inapokuwa nje.
Hivyo mashabiki wake, hata kama watakuwa wamenunua tiketi za msimu, lakini wamebaki kuwa walioonyesha mapenzi makubwa zaidi kwa timu yao kuliko wengine wote.  

Man United:
Uwanja wa Old Trafford una uwezo wa kuchukua watu 75,368 waliokaa kitako. Katika mechi ambazo Man United imefeli kuingiza watu wengi ni ile waliyoingia mashabiki 74,966 na imewahi kuingiza hadi watazamaji 75,185.
Kutokana na kuwa na mafanikio makubwa zaidi ya watazamaji walioingia uwanjani, Man United imefanikiwa kupata watazamaji 1,202,964.
Idadi hiyo kwa maana ya wastani, Man United inapata asilimia 99.88 ikiwa ndiyo timu yenye watazamaji wengi zaidi kuliko nyingine England msimu huu.
Wingi wa mashabiki wengi uwanjani ni kiasi gani mashabiki wanazithamini timu zao, ndiyo maana utaona hata Newcastle inakuwa juu ya Liverpool, Man City na Chelsea au Aston Villa kuwa juu ya Tottenham.

Arsenal:
Inaonekana kuwa na mashabiki wenye mapenzi ya dhati kwa kuwa wamekuwa wakiiunga mkono hata kama inayumba.
Msimu huu wana haki maana inaendelea kupambana tokea mwanzo wa msimu na wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kwenye Dimba la Emirates lenye uwezo wa kuchukua watu 60,071.
Emirates inaingiza watu 60,071 na mechi ambayo imeingiza watu wengi ni hiyo ya 60,071 wakati ile ambayo imeingiza watu wachache zaidi ni 41,598.
Jumla kabla ya mechi za wikiendi iliyoisha jana, watazamaji 941,891 wameingia kuishuhudia Arsenal ikicheza nyumbani na kwa asilimia ina 98.0, inashika nafasi ya pili baada ya Man United.

Newcastle:
Haifanyi vizuri sana kwenye Premiership, lakini ndiyo moja ya timu zenye mashabiki wengi zaidi England na hilo linadhihirishwa na takwimu za watazamaji.
Iko katika nafasi ya tisa katika timu 20 na mechi za mwisho zinaonekana kuwa si nzuri kwake.
Uwanja wake wa Saint James, unaingiza mashabiki 52,280 na kuna mechi imewahi kuingiza idadi hiyo, yaani hadi uwanja pomoni.  Jumla ya watu ambao wamewahi kuingia uwanjani hapo hadi leo ni  850,191.
Ingawa si maarufu nje ya England, lakini inashika nafasi ya tatu kwa mashabiki nchini humo na wastani wake ni asilimia 95.7.

Liverpool:
Hawa ndiyo wakongwe, moja ya timu zenye mafanikio makubwa na inashika nafasi ya pili kwa kubeba makombe ya Premiership na ilikuwa ina watazamaji wengi zaidi.
Lakini imekuwa ikifeli hadi kushika nafasi ya nane kwa kuingiza mashabiki licha ya kuaminika kuwa na mashabiki wenye mapenzi makubwa.
Lakini safari hii, ingawa haiko vizuri,  imejitutumua kufikisha jumla ya mashabiki 711,500.
Mechi ambayo timu hiyo imeingiza mashabiki wengi zaidi ni 44,882 na ndiyo idadi ya juu zaidi kwenye Uwanja wa Anfield ambao ni moja ya viwanja vikongwe vya soka duniani.

Man City:
Inashika nafasi ya tatu, kuna mabadiliko makubwa na imekuwa ikipanda kwa kasi sana kutokana na kufanya vizuri kwa misimu mitatu mfululizo sasa.
Uwanja wa Etihad una uwezo wa kuingiza watazamaji 47,364, ni kati ya timu chache za England ambazo msimu huu zilijaza watu pomoni wakati zikicheza.
Mechi ambayo imeshuhudiwa na mashabiki wachache zaidi ni ile waliyoingia 46,559. Hadi juzi imefanikiwa kushuhudiwa na watazamaji 706,594 na wastani wake ni aslimia 99.

Nyingine:

Hiyo ndiyo tano bora ya mashabiki walioingia zaidi kuzishuhudia timu zao zikiwa nyumbani, hata kama kutakuwa na wachache ambao wanatokea timu pinzani.
Timu nyingine tano zilizoingia kwenye kumi bora kwa mashabiki wengi kwenye viwanja vya nyumbani ni Chelsea iliyoshika nafasi ya sita kwa kuingiza mashabiki 705,341.

Nafasi ya saba ni Aston Villa yenye mashabiki 613,219 halafu Sunderland ambayo wameingia watu 609,103.
Kasi yao nzuri inawajenga Everton, maana wana jumla ya watazamaji 559,175 walioingia na Tottenham ndiyo inafunga kumi bora kwa kuwa na mashabiki 574,283.


  

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic