LIVERPOOL inaelekea ukingoni kwenye
kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England ikiwa na pointi 80 zinazoihifadhi kileleni.
Kama Liverpool itafanikiwa kushinda
mechi yake ya Jumapili ijayo dhidi ya Chelsea, maana yake itakuwa imemaliza kumla
ng’ombe mzima, mkia itakuwa ni kazi ya mwisho, ishindwe yenyewe.
Lakini hauwezi ukataja ilipofikia
Liverpool bila ya kumjumuisha bwa’mdogo Raheem Shaquille Sterling ambaye
amekuwa chachu ya mashambulizi ya kikosi hicho.
Kwa sasa, Sterling ni kati ya wachezaji
wanaoifanya safu ya ushambuliaji kuwa kali zaidi kuliko nyingine England, kwani
katika mechi 35 Liverpool imepachika mabao
96 ambayo ni mengi zaidi kufungwa kwa msimu huu. Man City inafuatia
ikiwa na mabao 96.
Sterling
aliyejiunga na Liverpool mwaka 2010 akiwa kinda kabisa ameshaichezea
timu hiyo mechi 57 na kufunga mabao 11. Na msimu huu ndiyo ameanza kuonyesha
kuwa ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa.
Asili yake ni Jamaica alikozaliwa miaka
19 jijini Kingston, Jamaica. Sterling aliyelelewa na bibi yake kabla ya kuhamia
England na mama yake akiwa na umri wa miaka mitano na taratibu alianza kuchukia
kisoka.
Sifa zake mbili kubwa ni kasi pamoja na
uwezo wa kuuhifadhi mpira na kujua nini cha kufanya tena kwa kasi kubwa.
Uwezo alionao na utofauti na wachezaji
wengine ndiyo ulimvutia Kocha Brendan Rodgers kuanza kumpanga hata katika mechi
ngumu huku baadhi ya wakongwe wa Liverpool wakipinga kwamba hakuwa ameiva.
Rodgers alipata ushindani mkubwa kwa
kuwa wakati alifikia wakati fulani alianza kumuweka nje Daniel Sturridge na
kumpanga Sterling ambaye alionekana kama alikuwa hana mchango.
Lakini katika mechi nane za mwisho
ambazo Liverpool imeshinda zote na kuwa timu yenye rekodi nzuri ya ushindi
mfululizo msimu, Sterling ndiye amekuwa kiongozi wa kuanzisha mashambulizi na
ikiwezekana kufunga mabao.
Miaka 19 tu, Sterling ameonyesha ana
uwezo mkubwa kwa kuwa katika dakika zake 1,960, tayari amekuwa tegemeo tena
akiwa na umri wa miaka 19 tu.
Takwimu zinaonyesha amepiga mashuti 33,
kati ya hayo 22 yamelenga lango huku mguu wake wa kulia ukionyesha kuwa ndiyo
una uwezo zaidi. Kwani katika mabao yake 9, sita amefunga kwa kulia na matatu
kwa kushoto.
Lakini ana kasoro kadhaa kama nguvu hasa
anapokutana na mchezaji mwenye nguvu na kasi, lakini ana uwezo wa chini sana katika
upigaji vichwa kwa kuwa hana hata bao moja la kichwa.
Kwa maana ya nidhamu ni mmoja wa
wachezaji wenye nidhamu ya juu uwanjani, kwani kwa msimu mzima ana kadi moja tu
ya njano. Wachezaji wenzake wamekuwa wakimsifia kwamba hata mazoezini ni
msikivu sana.
Lakini anashangaza wengi, kwamba nje ya
uwanja anaonekana anapenda sana ‘watoto’ lakini ana tabia za watu wa ‘Musoma’
za kuwatandika warembo anaokuwa na uhusiano nao.
Sterling anayelipwa kitita cha pauni
30,000 kwa wiki, amewahi kupandishwa kizimbani mara mbili kutokana na vituko
vyake vya kuwatandika wapenzi wake.
Miaka 19, tayari amepanda kizimbani mara
mbili kutokana na kuwapiga wapenzi wake wawili tofauti kwa nyakati tofauti.
Mara ya kwanzaalipandishwa kizimbani
mwaka juzi, lakini mambo yalipelekwa chinichini kutokana na umri wake kutofikia
miaka 18, watu wakamalizana ‘kibingwa’.
Mara ya pili ilikuwa Agosti 8, 2013
alikamatwa kwa kumdhalilisha mpenzi wake mwanamitindo na ilielezwa alimpiga,
lakini Septemba 20, mwaka huo, mahakama ikaamua kuwa hakuwa na hatia baada ya
kutokuwa na ushahidi.
Lakini bado amekuwa mtu wa mikasa, kwani
amewahi kupandishwa pia kizimbani kwa madai ya kukwepa kodi na ushiriki wake mdogo katika masuala ya
jamii.
Usimuona
ana umri mdogo au umbo dogo, Sterling ni baba wa mtoto mmoja wa kike
aliyezaliwa mwaka 2012 baada ya uhusiano wa muda mfupi tu na msichana ambaye
sasa si mpenzi wake.
0 COMMENTS:
Post a Comment