May 10, 2014



Na Saleh Ally
ACHANA kabisa na habari za kutimuliwa kwa Kocha David Moyes ambaye alipewa Manchester United baada ya kustaafu kwa Alex Chapman Ferguson.
Moyes ameiacha Manchester United katika nafasi ya saba, haijawahi kung’oka hadi leo na huenda ikaishia hapo kwa kuwe mwenye nafasi ya kuchukua nafasi ya sita ni Tottenham Hotspur.

Man United ina pointi 63, Spurs ina pointi 66 na kila moja ina mchezo wa kumaliza ligi kesho. Hivyo kama Spurs itapata sare tu kesho, basi Man United haitashiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.
Kawaida timu inayoshika nafasi ya tano na sita kwenye Premiership, inapata nafasi ya kushiriki Kombe la Europa. Jibu la Man United inabaki namba saba au la hadi mwisho wa ligi litajulikana kesho.
Pamoja na yote hayo, kinachoshangaza Manchester United kitakwimu inaonekana si timu iliyofanya vibaya sana kama ambavyo inaonekana kwa sasa ila kufeli sehemu kadhaa ndiko kunakoiangusha.
Mfano, kwenye msimamo iko katika nafasi ya saba, lakini ina tofauti kidogo sana ukiilinganisha na Arsenal ambayo iko nafasi ya nne na ina nafasi ya kuibakiza mkononi nafasi hiyo.
MABAO YA KUFUNGA:
Man United imefunga mabao 63, Arsenal ambao wako nafasi ya sita wana 66. Lakini mabao hao ya Man United ni mengi kuliko Everton iliyo nafasi ya tano, ina 59 na Spurs katika nafasi ya sita ina 52.
Utaona namna gani ambavyo Man United haina tofauti kubwa katika mabao ya kufunga na Arsenal ambayo iko mbali kwake kimsimamo, lakini namna ambavyo imezizidi timu mbili zilizo juu yake kwa ufungaji.
MABAO YA KUFUNGWA:
Kitakwimu, mabao machache ya kufungwa maana yake ni safu ngumu au bora ya ulinzi.  Man United imefungwa mabao 42 katika mechi zake 37, lakini kwa mechi idadi hiyo Arsenal wamefungwa mabao 42, bado tofauti ni kiduchu kabisa. Everton katika nafasi ya tano imeruhusu mabao 39.
Lakini bado safu ya ulinzi ya Man United ni bora hata kuliko timu zilizo juu yake kama Spurs iliyo nafasi ya sita, yenyewe imeshindiliwa mabao 51.
Sasa hapo ndiyo unaweza kujiuliza kwamba, kwa maana ya ubora wa kufunga na kufungwa haina tofauti na timu zilizo juu hasa nafasi ya nne kushuka chini, vipi imekwama?
ILIPOKOSEA:
Kikosi cha Man United chini ya Moyes kilikuwa bora katika kulinda kufungwa mabao machache na wakafanikiwa kufunga mengi, wamejitahidi. Tatizo lao lilikuwa ni kwenye pointi tatu.
Utaona katika msimamo, kinachoipandisha au kuishusha timu kutoka nafasi moja kwenda nyingine ni pointi na kawaida tatu ukishinda, moja ukipata sare.
Hesabu nzuri ilitakiwa kuwa ni kwenye mechi za kufunga na kufungwa. Vizuri kupoteza chache, kushinda nyingi na sare wastani, hapo ndiyo sehemu ya makosa makubwa ya Man United.
Utaona wakati wa Ferguson, hata kama itacheza vibaya vipi au kwa kiwango cha chini kupindukia, Man United itashinda 1-0 au kupata sare lakini si kupoteza pasi zake zote.
Msimamo baada ya mechi 37 unaonyesha Man United imeshinda mechi 19 tu, sare 6 halafu imepoteza mechi 12.
Kupoteza mechi 12 si kitu cha kawaida kwa Man United na isingekuwa na nafasi tena ya kukaa juu na kushindana na timu kama Man City, Chelsea na Liverpool ambazo kila moja imepoteza sita.
Sawa, hawapishani sana na Arsenal ambao  wamepoteza saba. Lakini ndicho hata kilichowadondosha vijana hao wa Arsene Wenger kwa kuwa wamepoteza mechi nyingi zaidi ya timu zilizo juu yake.
Man United iliyo chini ya Ryan Giggs ambaye ni mchezaji mkongwe na kocha wa muda sasa, isingekuwa na nafasi ya kujirekebisha kwa kuwa iliishachelewa basi. Lakini kocha yoyote atakayeinoa, lazima aingie kwenye falsafa ya Ferguson, kupoteza mechi chache na kupanda mbele, bora sare.
Kwa takwimu hizo, inaonekana kabisa Man United si timu yenye kikosi duni na hata kama marekebisho hayatakiwi kuwa makubwa kiasi cha kuvuruga, badala yake mhimili au kocha, ndiye anatakiwa kuwa imara zaidi mwenye dira na hesabu sahihi katika wakati mwafaka, ndiyo msimu utakuwa mzuri kwa Mashetani hao ambao msimu huu wamekuwa watu wa majonzi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic