Ligi Kuu
ya Bara kuanzia msimu wa 2015/2016 itakuwa na timu 16 badala ya 14 za
sasa.
Mabadiliko
hayo yamepitishwa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) iliyokutana jana (Mei 3 mwaka huu) jijini Dar es Salaam baada ya kupokea
mapendekezo ya kuongeza idadi ya timu kutoka kwenye Kamati ya Mashindano.
Uamuzi huo
umefanywa kwa lengo la kuongeza ushindani katika ligi hiyo, na kuwezesha
wachezaji kupata mechi nyingi zaidi za mashindano. Kwa mabadiliko hayo maana
yake ni kuwa Ligi ya msimu wa 2015/2016 itakuwa na mechi 240 wakati kwa sasa
ina mechi 182.
Kuhusu
idadi ya wachezaji wa kigeni kwenye VPL, Kamati ya Utendaji itafanyia uamuzi
mapendekezo katika eneo hilo baada ya kwanza kupata maoni ya klabu za VPL na
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambazo Mei 11 mwaka huu zitakutana na Rais wa TFF,
Jamal Malinzi.
Mapendekezo
ya Kamati ya Mashindano ni kuwa idadi ya wachezaji wa kigeni iendelee kuwa
watano kama ilivyo katika kanuni za sasa za VPL.
0 COMMENTS:
Post a Comment